MASHABIKI WAWATAKA VIONGOZI WA VILABU VYA JAMHURI NA KIZIMBANI KUBAKI LIGI KUU

October 17, 2013
Na Masanja Mabula -Pemba .
Hatimaye mashabiki wa vilabu vya Jamhuri na Kizimbani zote za mjini Wete, wamevunja ukimiya na kuuomba uongozi wa timu hizo kupanga mikakati itakayoziwezesha timu hizo kubakia kwenye michuano ya ligi kuu ya Zanzibar msimu ujao .

Wakizungumza kwa nyakati tofauti , wamesema kuwa mwenendo wa timu hizo kwenye ligi kuu ya Zanzibar inayoendelea sio wa kuridhisha , jambo ambalo limezifanya timu hizo kushika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi hiyo .

Aidha wameongeza kwamba huwenda  Mji wa Wete kukosa timu inayoshiriki ligi kuu msimu ujao  , endapo hatua za makusudi hazitrachukuliwa na viongozi wa timu hizo kwa kuweka mikakati madhubuti pamoja na kufanya usajili wakati wa dirisha dogo .

" Hii itakuwa ni aibu kwa Mji wa Wete kukosa timu ya kushiriki ligi kuu , na lwamba viongozi wa vilabu hivyo wanapaswa kufanya usajili wakati wa dirisha dogo litakapofunguliwa " alisisitiza shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina Omar Juma .

Wameeleza kwamba klabu hizo ambazo zinawawakilisha wananchi wa Mji wa Wete na Wilaya hiyo kwa ujumla , ambapo mikakati ya makusudi inahitajika ili kunusuri timu hizo kushuka daraja .

Kombo Said shabiki wa Timu ya Jamhuri alisema kuwa wanashangaa kuona timu yao imekuwa kichwa cha mwendawazimu tofauti na ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma ambapo ilikuwa tishio kwa vilabu vya ligi kuu Zanzibar .

"Matatizo ya timu yetu kufanya vibaya yamechangiwa na viongozi wetu kwa kukubali kuwatoa wachezaji zaidi ya sita wa kikosi cha kwanza na wao kushindwa kusajili wachezaji wa kuweza kuziba nafasi hizo " alieleza Kombo  .

Hata mmoja wa Viongozi wa Klabu ya Jamhuri ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema kuwa uongozi umekusudia kuvunja benki na kufanya usajili wa kutisha wakati wa dirisa dogo pindi likifunmguliwa .

Aliwatoa hofu mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo ,kuondoa wasiwasi na kwamba timu itaendelea kubaki kwenye ligi kuu Zanzibar kwani mapengo yalijitokeza katika kipindi hichi tayari wamo katika kuyapatia ufumbuzi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »