KOCHA JAMHURI ABWAGA MANYANGA

October 31, 2013


Na Masanja Mabula -Pemba .
Kocha Mkuu wa Timu  Jamhuri Said Mohammed ameamua kuikacha timu hiyo baada ya kudai kuwa hakuna utulivu ndani ya timu hali ambayo imepelekea kuweko na makundi kati ya Viongozi jambo ambalo limepelekea matokeo mabaya kwenye michuano  ligi kuu ya Zanzibar .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi , kocha huyo mwenye leseni ya daraja la C linalotambuliwa na Shirikisho la Mpira la Afrika ( CAF) amesema kuwa uwamuzi wa kuicha timu umekuja baada ya kuona kuwa baadhi ya viongozi wanahusika katika kuihujumu timu .

Amesema kuwa pamoja na mapungufu yaliyopo ndani ya kikosi cha timu hiyo Kongwe Visiwani hapa , lakini baadhi ya viongozi wamehusika moja kwa moja katika matokeo mabaya uwanjani .

"Haiwezekani kiongozi unasema kwa kuwaambia wachezaji kuwa tunnakwenda uwanjani kufungwa , badala ya kuwa wewe uwe ni chachu kuwahamisha wachezaji kufanya vizuri , kama sio hujuma ni nini mwandishi ? alihoji .

Aidha ameeleza kwamba kwa mujibu wa timu inavyocheza mpira uwanjani , hakuna sababu ya kuwa tushike nafasi ya chini kwenye msimamo , na kutokana na hali hiyo nimeona bora niachie ngazi kuonoa timu hiyo .

" Mimi nafanya kazi kwa bidii  , maarifa na nguvu zote , lakini kutokana na hali hii ndiyo maana nimeamua kuachia ngazi , naamini sasa viongozi watatambua kwamba hujuma zao hazilengi katika kuimarisha timu bali zinabomoa " alieleza .

Akizungumzia malengo yake ya badaye kocha Said amesema kuwa kwa sasa hana mpnago wa kufundisha timu kutokana ambapo anataka kutuliza akili yake baada ya kutumia muda mwingi katika klabu ya Jamhuri .

"Unajua nimetoka kufundisha timu yenye mashabiki wengi , kwa sasa siwezi kukurupuka na kuamua kutafuta timu ya kufundisha kwa kipindi hiki " alifahamisha .

Akizungumza na gazeti hili , Meneja wa Timu hiyo Abdalla Mohammed Elisha amekiri kupokea taarifa za kocha huyo kujiuzulu , na kuongeza kwamba sababu za kocha kuachia ngazi hazielewi .

"Ni kweli kocha wetu ameiacha timu kuanzia jana (juzi) lakini sababu zilizomfanya aiache timu mtafute na muulize yeye ,  mimi sizielewi na naamini ni uwamuzi wake mwenyewe "

Elisha amekanusha kwamba kocha huyo haelewani na baadhi ya viongozi wa timu hiyo na kwamba uwamuzi wa kuachia ngazi ni wake binafsi .

Tayari zipo taarifa kwamba kocha huenda akajiunga na timu ya Konde Star inayoshiriki ligi daraja la kwanza Taifa Pemba ambayo alikuwa anaifundisha kabla hajajiunga na timu ya Jamhuri .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »