COASTAL UNION WAENDELEZA DOZI YA MAZOEZI KUJIANDAA NA MSIMU MPYA.

July 20, 2013

Na Mwandishi Wetu,Tanga.
TIMU ya Coastal Union “Wagosi wa Kaya”leo imeendelea na mazoezi yake katika uwanja wa Mkwakwani mkoani hapa ikijiandaa na msimu mpya wa Ligi kuu Tanzania bara ambao utaanza mwezi ujao.

Mazoezi hayo ambayo yalianza majira ya saa nane mchana yalikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi na mshabiki mbalimbali wa soka mkoani hapa ambao mara nyingi hufuatilia mazoezi hayo kutoka pande zote za mkoa huu.
(KOCHA Mkuu wa Coastal Union Hemed Morroco kushoto akiteta jambo na Pius Kisambae huku Seleman Kassim Selembe akishuhudia)

Wachezaji ambao walionekana kuwakonga nyoyo mashabiki wa soka hapa wapenzi ni Haruna Moshi “Boban”,Christian Odula wa Nigeria,Jerry Santos,na wachezaji wengine chipukizi waliowasili kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza na Blog hii mara baada ya kumalizika mazoezi hayo,Kocha Mkuu wa timu hiyo,Hemed Morroco alisema maandalizi ya kuelekea msimu mpya yanaendelea vizuri kwani wachezaji wana hari na nguvu mpya.

Morroco alisema mechi ya kwanza ambayo atatumia kuangalia kikosi hicho ni kati yao na URA ya Uganda mchezo unaotarajiwa kucheza Jumatano wiki hii kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani hapa.
(Mashabiki wakifuatilia mazoezi ya timu hiyo leo jioni uwanja wa Mkwakwani)

Alisema watakapomaliza mechi hiyo wataelekea Mombasa Kenya kucheza na Bandari lengo likiwa kukipa makali kikosi hicho ambacho kimepania msimu ujao kuchukua kombe la Ligi kuu hapa nchini.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »