CCM Tanga wajiimarisha zaidi kuweza kurudisha kata tisa”

June 20, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga (CCM),Gustav Mubba amesema chama hicho kimejiwekea mikakati kabambe ya kuhakikisha wanarudisha kata tisa zilizochukuliwa na vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao 2015.

Pamoja na kata hizo lakini pia watahakikisha vijiji vyote vilivyochukuliwa na vyama vya upinzani vinarudi kwenye chama hicho kwani hilo linawezekana kutokana na uimara wa chama hicho.

Mubba alitoa kauli juzi wakati wa sherehe za kuwapongeza madiwani wapya wa CCM waliochaguliwa katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata za Genge na Tingeni wilayani Muheza na kueleza ushindi huo unaonyesha ni jinsi gani wananchi walivyokuwa na imani na mapenzi mema na chama hicho.

Alisema urudishwaji wa kata hizo katika chama hicho unawezakana kutokana na sera makini zinazotekelezeka pamoja na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopitia ambapo anaamini hilo litaweza kuwapa mafanikio ya kutimiza matarajio yao.

Aidha alielezea kufurahishwa na ushindi walioupata katika uchaguzi huo mdogo kutokana na upinzani uliokuwa ukionyeshwa na vyama vya upinzani ambavyo vilikuwa zikiwania nafasi hiyo.

Katibu huyo aliwataka makatibu wa wilaya katika chama hicho kuhakikisha wanawasimamia kikamilifu madiwani kufanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara. 

Aliwataka madiwani wa chama hicho kuhakikisha wanasimamia vyema ilani za chama hicho lakini pia aliwapongeza viongozi hao kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, Asha Mohamed alichaguliwa kuchukua nafasi ya udiwani kupitia chama hicho kwenye kata ya Tingeni na Mlaguzi Steven akichaguliwa kuchukua nafasi hiyo kupitia kata ya Genge iliyopo wilayani Muheza.

Akizungumza katika sherehe hizo, Diwani wa Kata ya Tingeni Asha Mohamed alisema atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na wananchi wa kata hiyo ili kuweza kuwapatia maendeleo pamoja na kuhamasisha vikundi vya ufugaji wa kuku ili wananchi wake waweze kujiajiri wenyewe.

Kwa upande wake, Mlaguzi Steven ambaye ni diwani wa kata ya Genge alisema atahakikisha anajipanga vilivyo na viongozi wengine kwenye kata hiyo ili kuwapa maendeleo wananchi wake.

Lakini pia Katibu Mubba alimtaka diwani wa kata ya Genge Mlaguzi Steven kuwa posho za baraza la madiwani zisimfanye amtekeleze mkewe wake.
  
   “Madiwani wakiwa wanagombea wanabembeleza sana, wakishinda hawatelezi ahadi zao,  watu wakishapata madaraka wanadharau wananchi wao sio tabia nzuri hivyo nawaasa mhakikishe mnawanyenyekea wananchi wenu na kuwa nao karibu “Alisema Mubba.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »