TAKUKURU TANGA YAOKOA FEDHA ZA SERIKALI MILIONI 76,048,459.1

February 06, 2025

 




Na Oscar Assenga,TANGA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefanikiwa kuokoa kiasi cha Milioni 76,048,459.1 baada ya kuwafikisha mahakamani waliokuwa watumishi wa umma kwa tuhuma za ubadhirifu na ufujaji wa Fedha za Umma katika wilaya za Kilindi, Korogwe na Tanga Jiji.

Tuhuma ambazo zilikuwa zinawakabili ni kutokuwasilisha fedha ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS na kuzitumia kwa manufaa yao pasipo kuwasilishwa sehemu husika kwa taratibu zilizowekwa.

Hayo yalisemwa leo na  Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Ramadhani Ndwatah wakati akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia mwezi Octoba hadi Desemba mwaka 2024.

Ambapo alisema kwamba baada ya kufikishwa mahakamani Jamhuri ilishinda kesi hiyo ambapo waliamriwa na mahakama kurejesha fedha kiasi hicho kwa mchanganuo mbalimbali.
Aidha alisema kwa wilaya ya Kilindi katika ufuatiliaji wa Jamhuri kushinda kesi za hujumu uchumi  namba 13,2023,11/2023 na 06/2024 dhidi ya watumishi ambao walishtakiwa kwa ubadhirifu kufuatia kutokuwasilisha fedha ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS na kuzitumia kwa manufaa yao pasipo kuwasilishwa sehemu husika kwa taratibu zilizowekwa.

“Fedha kiasi cha Sh Milioni 58,678,780.00 zilirejeshwa na watumishi hao kwa amri ya mahakama sambamba na adhabu nyengine “Alisema

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa alitaja wilaya nyengine kuwa wilaya ya Korogwe ambapo kiasi cha Milioni 9,198,045.31 ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS zilirejeshwa kwa amri ya mahakama kufuatia Jamhuri kushinda kesi za uhujumu Uchumi namba 09/2023 na 10/2023 dhidi ya watuhumiwa.

“Katika Jiji la Tanga Jamhuri ilishinda kesi za uhujumu uchumi namba 16558/2025 na 7/2023 ambapo Jumla ya Sh.Milioni 3,171,633.9 zilizofanyiwa ubadhirifu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya Elimu huku Milioni 5,000,000 ya mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu”Alisema.

Hata hivyo alisema kwamba fedha hizo zilirejeshwa na watuhumiwa kwa amri ya mahakama sambamba na adhabu nyengine .

“Tunatoa onyo kali kwa watu wote wanaofikiria kufanya hujuma ya aina yoyote katika matumizi ya rasilimali za umma  na tunawaasa waache tabia na fikra hizo mara moja na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya utendaji katika utumishi wa umma vyenginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”Alisema

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »