Na Oscar Assenga, Tanga.
ZAWADI kwa mshindi wa Redd’s Miss
Tanga 2013 anatarajiwa kuondoka na kitita cha sh.laki tano 500,000 huku msanii
wa muziki wa kizazi kipya, Tunda Man, akiongoza kwa upande wa Burudani, katika
shindano litakalofanyika Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa Mkurugenzi wa Kampuni ya DATK Intertainment Asha
Kigundula,alisema kuwa maandalizi ya shindano hayo yapo vizuri ambapo zawadi
kwa mshindi wa pili atajinyakulia kitita cha shilingi 300,000.
Kigundula
alisema katika shindano hilo mshindi wa tatu atazawadiwa kitita cha shilingi 250, 000 wakati mshindi wa nne na tano wakipata
sh.200, 000 kila mmoja na warembo wengine watakaosalia watapata kitita cha
sh.laki moja moja kila mmoja 100,000 kama kifuta jasho pamoja na zawadi kwa
mrembo mwenye nidhamu ili kuweza kuboresha shindano hilo.
Alisema kuwa hata hivyo kutakuwa na
zawadi kwa washindi watatu watakaoibuka katika shindano la vipaji (talent),
ambapo mshindi wa kwanza atainyakuliwa kitita cha shilingi 100,000 na mshindi
wa pili na watatu kila mmoja atajinyakulia shilingi 50,000.
Kwa upande wa Burudani msanii wa
kizazi kipya, Tunda Man, ataongoza safu ya burudani, ambapo itakuwa na wasanii
mbalimbali wakiwemo Dr John, Nabisha kutoka kundi la THT, Fady Dady na wasanii
chipukizi kutoka mkoani hapa.
Kigundula alisema shindano hilo
linatarajiwa kuanza majira ya saa mbili usiku na kushirikisha warembo 12 ambao
watachuana ili kuweza kumpata malkia wa mkoa huu ambaye atauwakilisha mkoa
katika mashindano hayo ngazi ya kanda.
Warembo hao ni Hawa Ramadhani
(18),Hazina Mbaga (19)Like Abdulraman (19), Irene Thomas(20), Tatu Athumani
(19), Winfrida Gutram (21)Lulu Mbonela (19) ,Hazina Daniel (19),Lulu
Matawalo(22),Judithi Moleli (21),Neema Jonas na Hawa Twaybu(21)
Wakati huo huo Warembo hao wanaowania
Taji la Mlimbwende wameiomba Halmashuri ya Jiji la Tanga kuifanyia marekebisho
barabara inayokwenda katika mapango ya Amboni ili iweza kuwa nzuri na ipitike
kirahisi nyakati zote.
Ombi hilo lilitolewa na warembo hao
mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea mapango hayo ambapo walikwenda
kujifunza histori yake pamoja na kuingia mapangoni lengo likiwa ni kujifunza
utalii wa ndani ili kuweza kuuutangaza kwa wageni na jamii nzima.
Akizungumza mmoja wa warembo hao,
Asia Rashid alisema mapango hayo ni mzuri na endapo yatafanyiwa maboresho
ikiwemo kufanyiwa ukarabati barabara inayoelekea katika kivutio hicho
itarahisisha usafiri na kupitika bila shida nyakati zote.
Asia alisema wao kama washiriki wa
shindano la Redd’s Miss Tanga 2013 wamefarijika sana kupata nafasi ya
kutembelea mapango hayo na kuwataka wananchi wa mkoa wa Tanga na wageni
wanaoingia mkoani hapa kuwa na utaratibu wa kutembelea vivutio hivyo na
kujifunza mambo mwengi ya kale.
Kwa upande wake, Hawa Ramadhani
aliwashauri watanzani kujenga utamaduni kutembelea vivutio vya utalii hapa
nchini ikiwemo kutunza misitu yetu ili nchi yetu ipendeze na kuwavutia wageni
wanaoingia hapa nchini kutoka mataifa mbalimbali.
Hawa alisema wao wamejipanga vema
kuhakikisha wanafanya vizuri katika fainali ya shindano hilo ambalo litafanyika
June 22 mwaka huu kwenye uwanja wa mkwakwani mkoani Tanga na kushirikisha
warembo.
Mwisho.
EmoticonEmoticon