Na Oscar Assenga, Tanga.
MABINGWA wa Ligi kuu Tanzania Bara
mwaka 1988 African Sports “Wanakimanumanu” inatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa
uchaguzi Agosti 15 mwaka huu baada ya uongozi wa muda uliopo madarakani
kumaliza wakati wake.
Akizungumza na blog hii, Katibu Mkuu wa
Klabu hiyo, Khatibu Enzi alisema uchaguzi huo unafanyika kutokana na kuongozwa
na viongozi wa muda hivyo wakapendekeza kuitishwa mkutano huo ambao utatoa
mwelekeo wa kuwapata watendaji wapya ambao watakuwa na jukumu la kuingoza klabu
hiyo.
Enzi alisema fomu za kuwania nafasi
katika uchaguzi huo zitaanza kutolewa kuanzia Julai 2 mwaka huu kwenye makao
makuu ya klabu hiyo zilizopo barabara 12 jijini Tanga baada ya kikao cha kamati
ya utendaji wanachama wao.
Katibu huyo alizitaja nafasi ambazo
zitagombewa katika uchaguzi huo kuwa ni nafasi ya mwenyekiti, makamu
mwenyekiti, katibu mkuu, katibu msaidizi, mweka hazina na msaidizi wake huku
nafasi kumi za wajumbe watakaounda kamati ya utendaji wa klabu hiyo nazo zikiwaniwa.
Aidha katibu huyo alisema kuelekea
uchaguzi huo wanatarajiwa kutoa fomu mpya za uanachama kwa wanachama wapya
ambao wanataka kujiunga na klabu hiyo ambazo zitatoka kuanzia June 22 mpaka
Julai 30 mwaka huu.
Mwisho.
EmoticonEmoticon