MKURUGENZI wa Jiji aifunda timu ya Umitashumta Tanga

June 20, 2013
 Na Oscar Assenga,Tanga.
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Juliana Malange ameitaka timu ya Mkoa wa Tanga ya Umitashumta kuhakikisha inauwakilisha vema mkoa katika mashindano ya kanda na kuweza kurudi na kombe la michuano hiyo.

Malange alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa ufungaji wa mashindano hayo ngazi ya mkoa ambayo yalifanyika katika viwanja vya shule ya ufundi ya Tanga School na kuhudhuriwa na wanamichezo 900 ambao walishiriki michezo mbalimbali.

Mkurugenzi huyo alisema michezo inafaida nyingi sana katika maisha ya kila siku ikiwemo kuwaepusha vijana kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na ulevi wa aina yoyote na ngono zembe kwa kuwa mambo hayo huaribu kabisa ndoto ambazo wamejiwekea maishani na kudhoofisha nguvu kazi ya taifa.

Aidha alisema anaimani kubwa na wanamichezo 122 ambao wamechaguliwa kuuwakilisha mkoa kwenye mashindano ya Umitashumta ngazi ya Kanda watafanya vizuri na kuwataka kupambana vilivyo ili kuuwakilisha vema mkoa wa Tanga ambapo kati yao wavulana 71 na wasichana 51.

“Ninaimani kuwa timu iliyochaguliwa kuuwakilisha mkoa kwenye mashindano ngazi ya kanda itakuwa ni nzuri, napenda kuwatakia kila heri lakini mfahamu kuwa mmepewa dhamana kubwa ya kuuwakilisha mkoa hivyo hakikisheni mnawapa raha wakazi wa mkoa huu “Alisema Malange.

Pia aliwataka walimu wanaosimamia wachezaji hao katika michezo mbalimbali wahakikishe wanaongeza juhudi kwenye kila mchezo ili kuweza kuchukua ushindi wa jumla kwenye mashindano hayo.

Mkurugenzi huyo alimshukuru na kumpongeza rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete kwa hatua yake ya kurudisha michezo mashuleni na hivyo kuwafanya wanafunzi wa shule mbalimbali hapa nchini kushiriki michezo kupitia mashindano hayo.Hata hivyo aliwataka walimu hao kuwa karibu na wachezaji wao ili waweze kufahamu changamoto zinazowakabili na kuweza kuzifanyia kazi kwa wakati ikiwemo kuwapa hamasa kufanya vizuri.

Lakipi pia aliwataka wachezaji hao kuzingatia kauli mbiu ya mashindano ya umitashumta 2013 isemayo “Michezo na utulivu kwa maendeleo ya Taifa”huku akiwasisitiza walimu na viongozi kuhakikisha wanakuwa karibu na wachezaji wakati wote ili kujua matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi mapema.


Mashindano hayo msimu huu yalishirikisha michezo ya mpira wa miguu,mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana,mpira wa pete wa wasichana,mpira wa wavu wavulana na wasichana na michezo yote ya riadha.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »