DKT.MATARAGIO AONGOZA WADAU UTOAJI MAONI MPANGO WA MATUMIZI YA GESI ASILIA NCHINI (NGUMP)

October 07, 2025 Add Comment



*📌Unalenga Kuchochea matumizi ya Gesi Asilia nchini*


📌 *Kuainisha matumizi ya Gesi Asilia kwa sekta mbalimbali katika kipindi cha miaka 25 kuanzia sasa*


*📌Kuangazia masoko ya Gesi Asilia ndani na nje ya nchi*


*📌Wadau waomba uharakishaji mikopo kwa wawekezaji Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia*



 *DSM* 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amefungua warsha ya wadau iliyolenga kuchambua na kutoa maoni kuhusu Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia nchini (NGUMP) kwa kipindi cha miaka 25 kuanzia sasa.


Mpango huo utaonyesha kiasi halisi cha matumizi ya gesi asilia kinachohitajika katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika sekta ya viwanda, uzalishaji wa umeme, sekta ya usafirishaji pamoja na matumizi ya nyumbani


Warsha hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam imeandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na kuhusisha wadau kutoka serikalini, sekta binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.

"Mradi huu wa  NGUMP utatuwezesha kufahamu kiasi halisi cha matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali hivyo itakuwa rahisi kufahamu na kutenga kiasi cha gesi asilia inayohitajika katika eneo husika," amsema Dkt. Mataragio


Ameongeza kuwa NGUMP itasaidia kuona namna bora ya kuendeleza miundombinu ya gesi ya asilia nchini pamoja na kutafuta masoko ya gesi asilia ndani na nje ya nchi pia kuangalia mchango wa gesi hiyo  katika uchumi wa nchi.


Vilevile amesema NGUMP itarahisisha utekelezaji wa DIRA ya Maendeleo ya 2050 kwa kuwa Gesi asilia ipo katika Sekta ya Nishati ambayo ni kichocheo cha pili Kati ya vitano vya kufanikisha matokeo  ya Dira.

Aidha amesema NGUMP itatekeleza mpango mkakati wa Matumizi Nishati Safi ya Kupikia na Sera ya Nishati ya mwaka 2015.


Mhandisi John Bura ni mmoja ya washiriki katika warsha hiyo ambaye amesema kuwa  mpango huo utasaidia kuchochea matumizi ya gesi asilia, pamoja na kuongeza kiwango cha matumizi ya gesi nchini.


Bura ameiomba Serikali pamoja na Taasisi za Fedha kuharakisha utoaji wa mikopo kwa wawekezaji hasa wa ndani wanaotaka kuwekeza katika maeneo mbalimbali kwenye sekta hiyo ili kusogeza huduma hiyo kwa wananchi kwa lengo la kupata matokeo mazuri yenye tija zaidi.



Hatua ya utoaji utoaji maoni ya NGUMP imefikwa baada Wizara ya Nishati na JICA kukamilisha rasimu ya NGUMP kupitia Mradi wa kujenga uwezo katika matumizi ya Gesi Asilia na kuongeza uzalishaji.

TTCL YASEMA "HAKUNA LISILOWΕΖΕΚΑΝA" ΚΑΤΙΚΑ KUTOA HUDUMA BORA

October 06, 2025 Add Comment


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025, likiahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa ubunifu, kasi na ufanisi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania na wateja wake wa kimataifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa wiki hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kujitathmini na kuimarisha uhusiano kati ya shirika hilo na wateja wake.

“Wiki hii inatukumbusha wajibu wetu wa msingi wa kumweka mteja mbele kama kiini cha mafanikio ya TTCL. Tunajitathmini, tunasikiliza, na tunajifunza kutoka kwa wateja wetu,” amesema Bi. Moshi.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja hufanyika duniani kote kila mwaka wiki ya kwanza ya Oktoba. Kwa mwaka huu, TTCL inasherehekea kuanzia Oktoba 6 hadi 10, 2025 chini ya kaulimbiu isemayo “Mission: Possible.”

Bi. Moshi amesema kaulimbiu hiyo imechaguliwa kuonyesha dhamira ya TTCL ya kuona kila changamoto kama fursa ya kuboresha huduma na kutafuta suluhisho la kudumu kwa manufaa ya wateja.

“Tutakuwa wabunifu, wenye bidii na maono. Kila mmoja wetu atakuwa sehemu ya suluhisho, na kwa pamoja tutahakikisha kila mteja anathaminiwa na kuhudumiwa kwa ubora wa hali ya juu,” amesisitiza.

Amesema TTCL imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini, ikiwa ni pamoja na kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi kufikia wilaya zote za Tanzania, pamoja na ujenzi wa minara 1,400 vijijini ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano bila vikwazo.

Aidha, amesema kupitia huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako”, TTCL inaendelea kuwapatia Watanzania huduma ya intaneti ya kasi na uhakika inayokidhi viwango vya kimataifa.

Bi. Moshi ameongeza kuwa TTCL itaendelea kuwekeza katika teknolojia bunifu, kuboresha mifumo ya huduma kwa wateja na kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora popote walipo.

Amewahimiza wateja waendelee kutumia Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachofanya kazi saa 24, pamoja na mitandao ya kijamii na maduka ya TTCL nchini kote, kupata ushauri na taarifa muhimu.

“Tutaendelea kuwa karibu na wateja wetu, kuwaheshimu, na kuhakikisha wanapata huduma bora zenye ufanisi na thamani,” amesema.

Bi. Moshi amewashukuru wateja wote walioliweka TTCL kama chaguo lao la mawasiliano kwa miaka mingi na kuwataka waendelee kushirikiana na shirika hilo katika safari ya maendeleo ya kidijitali.

“Wateja wetu ndiyo msingi wa mafanikio yetu. Tutaendelea kuwa bega kwa bega nao kufanikisha azma yetu ya pamoja — Mission: Possible,” alisisitiza kabla ya kutangaza rasmi uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja ya TTCL kwa mwaka 2025.







WANANCHI WA IYAGABUYA GA-BUSEGA WAASWA KUFUATA SHERIA ZA UHIFADHI WANYAMAPORI

October 06, 2025 Add Comment



Na Mwandishi Wetu, Simiyu


Serikali imewaasa wananchi wa Kijiji cha Iyagabuyaga, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu kufuata sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi wa wanyamapori ili kuepuka migogoro na Serikali pamoja na kuendeleza shughuli za uhifadhi endelevu nchini. 


 Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Nassoro Wawa ameyasema hayo Oktoba 6, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi na namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu, kufuatia tatizo la fisi lililokithiri katika eneo hilo.

Katika utoaji elimu hiyo unaofanywa na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, TAWA, na Maafisa Wanyamapori wa Halmashauri mkoani humo, Afisa huyo amesema Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori,  inasema kuwa mnyama ni nyara ya Serikali, na ukikamatwa huna kibali ni kosa la uhujumu uchumi."

Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi kisheria, ikiwemo kuanzisha bucha za wanyamapori, bustani, mashamba na ranchi za wanyamapori, hatua inayolenga kuchochea maendeleo na kuongeza kipato kwa wananchi.

“Sheria hizi zimekuja kumuwezesha mwananchi kunufaika na rasilimali za wanyamapori nchini ambazo ziruhusu mwananchi,  kikundi, kijiji kuanzisha bucha ya nyamapori, bustani, shamba na ranchi za wanyamapori ili kuinua kipato na kuleta maendeleo tunayoyataka,” amesisitiza.


Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),  Lusato Masinde, amebainisha kuwa wananchi wanaruhusiwa kumuua mnyamapori anapothibitishwa kuwa tishio kwa maisha au mali, lakini kwa sharti la kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa Serikali.

 “Kama mnyamapori atahatarisha maisha au mali zako, unaweza kumuua lakini lazima utoe taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Mtendaji au Maafisa Wanyamapori. Nyara hizo ni mali ya Serikali na lazima zikabidhiwe sehemu husika,” ameeleza  Masinde.

Aidha, ameonya kuwa mtu yeyote atakayemuua mnyamapori bila kutoa taarifa kwa mamlaka husika atakuwa ametenda kosa na kufuatana na sheria atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi na akithibitika atahukumiwa kifungo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Iyagabuyaga, Bw. Bahati Masaga, amesema changamoto ya fisi imekuwa kubwa kijijini hapo, na Serikali ilifanikiwa kuwaua fisi 17 hivi karibuni.


Ameishukuru Serikali kwa kutoa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na kuahidi wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kutatua tatizo hilo na kuwaomba waachane na imani potofu za kishirikina za kufuga fisi. 


&&&

MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU :MVUTANO WA AINA YAKE AFRIKA

MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU :MVUTANO WA AINA YAKE AFRIKA

October 06, 2025 Add Comment

 

Mijadala kuhusu uhuru wa maamuzi na maadili barani Afrika inazidi kupamba moto, na Tanzania iko katikati ya mvutano wa kitamaduni wa kimataifa. Swali kuu linabaki: Nani anaamua jamii iishi vipi?

Kwa Umoja wa Ulaya (EU), jibu ni moja — haki za binadamu ni za wote, na usawa wa watu wenye mwelekeo wa jinsia au utambulisho wa kijinsia tofauti na ule wa kawaida wa kijamii unapaswa kulindwa kila mahali. Kwa Tanzania, viongozi na chama tawala CCM, jibu linapatikana katika misingi ya maadili, mila, na utamaduni wa kizazi kwa kizazi.

Mnamo Januari 2025, Huduma ya Utafiti ya Bunge la Ulaya ilisisitiza msimamo wa EU wa kuendeleza haki za jinsia na mwelekeo wa kijinsia duniani. Hata hivyo, ilikiri changamoto kwamba makubaliano na mataifa ya Afrika mara nyingi hayaelezi wazi masuala ya kundi hilo ili kuepuka mgongano wa kisiasa.

Wakosoaji nchini Tanzania wanaona hatua hiyo kama njama ya kifedha kupitia miradi ya mashirika yasiyo ya kiserikali, ikipuuza mahitaji muhimu kama afya, barabara na elimu.

Rais Samia Suluhu Hassan, alipowasilisha sera ya mambo ya nje mwezi Mei 2024, alionya wanaharakati wa kanda wasiingilie mambo ya ndani ya nchi. “Tusiruhusu Tanzania iwe shamba la bibi kwa kila anayepita kutoa tamko,” alisema.

Wakati huohuo, ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya 2024 ilionya kuhusu kupungua kwa uhuru wa kiraia na ongezeko la vitisho kwa wanaharakati na makundi yaliyotengwa, ikihimiza serikali kuoanisha sheria na viwango vya kimataifa. Serikali ilipinga ikisema ripoti hizo zinachochewa na ajenda za nje zinazotishia amani ya taifa.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisisitiza kwamba kurejesha maadili ni jukumu la jamii nzima. “Kila taasisi inapaswa kushiriki katika kuimarisha maadili ya taifa,” alisema, akieleza kuwa wizara yake inaendeleza mwongozo wa malezi ya watoto unaolinda maadili ya Kitanzania.

Katika muktadha wa Kiafrika, familia ni zaidi ya wazazi na watoto; ni msingi wa utamaduni na nidhamu ya kijamii. Mpango wa Maendeleo wa Halmashauri ya Kilombero (2021–2026) unasema kuporomoka kwa familia kunaleta kuporomoka kwa maadili na milango kwa ushawishi wa nje.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye Maulid Kitaifa Tanga, alisema Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, uzalendo na maadili mema. “Maisha ya Mtume yanatufundisha kuishi kwa maadili na kutegemea Mungu,” alisema, akisisitiza kulinda amani kama zawadi ya kiungu.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali, aliwataka viongozi wa dini kuimarisha mahubiri dhidi ya vitendo vinavyohatarisha amani, akisema, “Amani si hiari, kila mmoja ana wajibu wa kuilinda.”

Kwa serikali, maadili si suala la kidini tu bali ni msingi wa usalama wa taifa. Ndiyo nguzo ya ibada, maisha ya kila siku, na maendeleo.

Mjadala huu umeingia pia katika siasa. Wagombea wa upinzani, kama Hassan Almas wa NRA na mgombea wa ADC, wameahidi sheria kali zaidi dhidi ya ushoga — ishara kuwa hoja hii imekita mizizi kwenye uwanja wa kisiasa.

Tanzania inaungana na mataifa mengine ya Afrika kama Ghana na Uganda, yanayopinga kile kinachoitwa “uenezi wa tamaduni za Magharibi.” Kwa CCM, kulinda amani na maadili ya ndani ni ushahidi wa ufanisi wa misingi ya taifa.

Kutoka falsafa ya Ujamaa ya Nyerere, misimamo ya Magufuli, hadi diplomasia ya Samia, msimamo unabaki uleule — Tanzania inaamua yenyewe jinsi jamii yake inavyoishi.

Na hivyo swali linaendelea kuzungumzwa kwenye ofisi, makanisa, misikiti na vijijini kote: Nani anaamua jamii iishi vipi?

WANANCHI BUNDA WAISHUKURU SERIKALI UJENZI WA VIZIMBA VYA KUZUIA MAMBA

October 06, 2025 Add Comment

Wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kuwajengea vizimba vya kuzuia mamba kuwadhuru wakati wa kuchota maji ziwani na kufanya shughuli zingine pembezoni mwa Ziwa Victoria ikiwemo kufua na kuoga.

Wamesema hayo leo Oktoba 6, 2025 kwa nyakati tofauti wakati timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea maeneo ya vizimba hivyo.

Akizungumza katika ziara hiyo,Mkazi wa Mwiseni,kata ya Butimba, Bi. Gabaseki Gervaz  amesema wamefurahi sana kupata kizimba kutokana na changamoto walizokuwa wanakutana nazo mwanzoni za kukamatwa na mamba wanapofanya shughuli zao pembezoni mwa ziwa.

"Serikali baada ya kuona tunateseka kutokana na vifo kila mwaka kwa kuuliwa na mamba ikajenga kizimba hiki" amesema Bi. Gervas na kuiomba Serikali kuongeza vizimba vya ziada kwa ajili ya jinsia ya kiume na mifugo.

Naye, Bw. Tabingwa Charles Kasao mkazi wa kitongoji cha Nampangala kata ya Kisorya ,Bunda mkoani Mara ameishukuru Serikali kwa kujali wananchi na kujenga kizimba katika eneo hilo na kuepusha vifo vya wananchi wakiwemo wanafunzi wanaotumia ziwa hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni, Bw. Msiba Chiharata amesema kutokana na faida za vizimba katika kuzuia mamba wanaodhuru wananchi, wameweka adhabu kwa wananchi wanaojaribu kuharibu eneo la Kizimba.



"Tumeweka adhabu kwa mtu yeyote atakayefanya uharibifu wa aina yeyote ile iwe ni kuanika nguo au kuingiza mifugo eneo la vizimba faini ni shilingi laki moja" amesema Bw.Msiba.