MAPOKEZI YA DKT.NCHIMBI NDANI YA JIMBO LA KISESA,MEATU AKIENDELEA NA MIKUTANO KUOMBA KURA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

September 02, 2025 Add Comment



MAMIA ya Wananchi  wa Kata ya Mwandoya ndani ya Jimbo la Kisesa,wilayani Meatu wakimsikiliza  Mgombea Mwenza wa Urais wa   Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi  wakati akiwahutubia kwenye mkutano wa hadhara leo Septemba 2,2025,wakati akiendelea na Mikutano yake ya Kampeni mkoani Simiyu.

Katika mkutano huo wa kampeni,Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi alimnadi Mbunge wa Jimbo hilo la Kisesa,Musa Godfrey Mbuga pamoja na diwani wa kata ya Lubiga,Juma Mpina ambaye ni kaka wa mbunge wa zamani wa jimbo laKisesa, Luaga Mpina

Pamoja na mambo mengine Balozi Dkt.Emmeanuel Nchimbi amekuwa akiinadi Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030,ambayo kimsingi imelenga kwenda kuboresha maisha ya wananchi na ustawi wa Maendeleo katika miaka mitano ijayo huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumchagua mgombea Urais wa CCM Rais Dk.Samia Suluhu,Mgombea mwenza wa Urais,wabunge na madiwani wa Chama hicho.




TUMEKUJA KUSIKILIZA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI BUKOMBE MKOANI GEITA

September 02, 2025 Add Comment

Makundi mbalimbali ya Wananchi wakiwa tayari kusikiliza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025-2030  kupitia Wagombea Ubunge na Udiwani Mkoa wa Geita ikiwa leo ni siku ya uzinduzi wa Kampeni za CCM mkoani Geita  kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

#ChaguaCCM

#OktobaTunatiki

#MchagueSamia

#MchagueBiteko

#KusemaNaKutenda

#KaziNaUtuTunasongaMbele

SERIKALI INA MPANGO WA KUONGEZA UWEKEZAJI SEHEMU YA KUTOA HUDUMA BANDARI YA TANGA

September 02, 2025 Add Comment


Na Oscar Assenga, TANGA



SERIKALI imesema kwamba ina mpango wa kuendelea kufanya uwekezaji katika Bandari ya Tanga kwa kuongeza sehemu ya kutoa huduma mara mbili kutoka mita 450 hadi kufikia mita 900 ili kuendelea kuongeza ufanisi wa kuhudumia shehena



Hayo yalibainishwa Septemba 1,2025  na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakati alipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kuona uwekezaji uliofanywa na Serikali wa Sh.Bilioni 429.1, huku akiridhishwa na maboresho yaliyofanyika ambayo yameiwezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Alisema kwamba uwekezaji katika Bandari hiyo utaendelea kuwa chachu ya kuongeza matokeo ya wazi ya kiuchumi kutokana na kuchangia uwepo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na hivyo kuchangia maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.

Aidha alisema kwamba katika sehemu ya kutolea huduma kuna mita 450 na kina mita 3 na kinaenda kuwa mita 13 ikiwemo lango la kuingilia limepanuliwa na kufikia upana mita 135 kwa kina cha mita 13 lakini bado kuna mipango inafanyika kuongeza ifike mita 900.

“Tunaiona Bandari hii ikichangamka tayari Serikali inakwenda kufanya uwekezaji mara mbili kutoka mita 450 mpaka mita 900 maana yake ni mita ni 1800 sasa unapokuwa unaangalia maeneo ya Bandari uwekezaji huo na ule uwekezaji wa Chongoleni kwa ajili ya mafuta ukiangalia gati inayotengenezwa kwa ajili ya Meli kubwa zinazokuja kusafirisha mafuta ghafi yanayotoka nchini Uganda huu ni uwekezaji mkubwa ”Alisema



Aliongeza kwamba maana tayari eneo la Tanga litakuwa ni kitovu cha biashara pamoja na eneo ambalo kila mtu kutoka mataifa mbalimbali atakuwa anaifahamu na kuwa na uwekezaji mkubwa na kuleta nafasi kubwa za kiuchumi sio kwa mkoa bali nchi nzima.

“Kimsingi mimi kama Msimamizi wa Mashirika na Mmiliki kwa niaba ya Serikali ninafarijika na huduma zinazotolewa na TPA na utulivu tunauona uimara wa huduma maana yake ni muunganiko wa vitu viwili uongozi inayofahamu kazi yake na watumishi wanaofanya kazi yao kwa ustawi wa juu”Alisema



Alisema kwamba wanazidi kuwa na matumaini makubwa sana kwa sababu Bandari asilimia kubwa ya mapato yake yanayokusanywa na TRA wanatoka Bandari na wanafikiria ni muhimu kuendelea kuitazama Bandari kwa jicho la Pekee.

“Lakini niwasihi wafanyakazi wa Bandari tuone ufahari tupo sehemu ambayo ni jicho na mboni ya Serikali katika uchumi wa nchi kwa hivyo lazima tuichukulie kama sehemu muhimu inayohitaji huduma zilizobora na tija kwa ajili ya maendeleo”Alisema



Hata hivyo alisema kwamba jambo jingine ni kuendelea kuhakikisha sekta binafsi na umma zinaungana lakini mali inabaki kuwa ni ya Bandari na zitabali kuwa mali ya nchi na wananchi kwa ujumla.

“Tunachokizungumza hapo ni na wanachokizungumza ni wawekezaji ambao watakuja kuziendesha na watapata mapato lakini baada ya muda kile kitu ni mali yetu na hakiondoki na maana yake tunakuwa na ushindani na ufanisi na huduma zitaendelea kuwa bora hivyo ni jambo la msingi na watanzania waendelea kujiunga na kujifunza kwa waliokuja kuwekeza”Alisema



Awali akizungumza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa alisema uwekezaji wa viwanda huo umesaidia kuhudumia meli kwa urahisi na gharama nafuu kutokana na kuimarika miundombinu ya Bandari ya Tanga



“Sisi tumekusanya Bilioni 75 ambazo tunatumia kulipa wafanyakazi,vifaa na kufanya ukarabati tunatumia fedha hizo Tanga kuna ukuaji mkubwa wa viwanda na kichosabababisha ni Bandari sasa tunaweza kuhudumia meli kwa urahisi na bei nafuu ndio inapeleka uwekezaji wa viwanda”Alisema

Hata hivyo alisema ujenzi viwanda vilivyo vinasababisha ukuaji wake kuimarika kwa Bandari ikiwemo maboresho walioyafanya na ukuaji wa uchumi na mahitaji na maendeleo yanazidi kufanywa ikiwemo upanuzi zaidi na watajenga mita 900 zaidi.

“ Leo utaona kuna meli mbili zinahudumiwa na meli tatu nje zinasubiri hivyo tunahitaji kupanua miundombinu ili kuweza kuzihudumia meli zote kwa wakati na kuwasaidia wafanyabiashara na wakulima kulifikia soko kupitia Bandari ya Tanga”Alisema

Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha alimhakikishia Msajili huyo kuwa huduma katika Bandari ya tanga itazidi kuimarika kwa maana ya kwamba meli zitakapokuwa zinakuja watazihudumia sio kwa zaidi ya siku tatu meli inaondoka huku akitoa wito kwa watumiaji wa Bandari hiyo waendelee kuitumia

MGOMBEA URAIS WA NLD MHE .DOYO HASSAN APOKELEWA KWA DUA NA WAZEE WA MISIMA HANDENI

September 02, 2025 Add Comment

HANDENI, TANGA 


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, amepokelewa kwa heshima ya kipekee na kufanyiwa dua maalum na wazee wa Kijiji cha Misima, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.

Wazee wa kijiji hicho walijitokeza kwa wingi kumpokea Mhe. Doyo na kumfanyia dua za kumtakia kheri, baraka, na mafanikio katika safari yake ya kisiasa ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Misima, mmoja wa viongozi wa kidini alisema, “Misima ni sehemu yenye historia kubwa ya mapambano ya ukombozi wa taifa hili. Tunamwona Mhe. Doyo kama kijana aliyepita katika nyayo zile zile za wazee wake waliopigania uhuru. Uthubutu wake ni wa kipekee na utakumbukwa na vizazi vijavyo hapa Misima.”

Kwa upande wake, Mhe. Doyo aliwashukuru wazee hao kwa mapokezi yao yenye heshima na maombi yao ya baraka.

JKT  YAADHIMISHA MIAKA  61 YA JWTZ  KWA KUCHANGIA DAMU SALAMA KWA JAMII,KUPANDA MITI NA KUFANYA USAFI KIKOSINI

JKT YAADHIMISHA MIAKA 61 YA JWTZ KWA KUCHANGIA DAMU SALAMA KWA JAMII,KUPANDA MITI NA KUFANYA USAFI KIKOSINI

September 01, 2025 Add Comment

 

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele,akiwaongoza  Maafisa ,Askari na Vijana kupanda miti  katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT, pamoja na kuchangia damu katika Hospitali ya Uhuru, Chamwino jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 61 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuasisiwa kwake Septemba 1, 1964, 

Na.Alex Sonna-CHAMWINO

KATIKA kuadhimisha miaka 61 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuasisiwa kwake Septemba 1, 1964, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, ameongoza Maafisa ,Askari na Vijana kupanda miti ya katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT, pamoja na kuchangia damu katika Hospitali ya Uhuru, Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza katika maadhimisho hayo leo Septemba 1,2025 , Meja Jenerali Mabele ametoa wito kwa taasisi mbalimbali nchini kujitokeza kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo muhimu.

Amesema  kwa maelekezo ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, vikosi vyote vya JWTZ vimeadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kupanda miti, kufanya usafi na kuchangia damu katika maeneo yanayowazunguka.

“Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania ni mali ya wananchi, hivyo katika sherehe hizi ni lazima turudi kwa jamii. Sisi JKT tumeona tujitolee damu kwa wahitaji, tukitambua uhitaji ni mkubwa,” amesema  Meja Jenerali Mabele.

Ameongeza kuwa vijana wa JKT wamejitokeza kuchangia damu kutokana na kutambua uhitaji mkubwa uliopo hospitalini. Aidha, amewaongoza Maafisa Askari na Vijana kupanda miti ya kumbukumbu katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kambi Makao Makuu ya JKT, Kanali Geofrey Mvula, amesema pamoja na kupanda miti na kuchangia damu, pia elimu imetolewa kwa Maafisa, Askari Vijana kuhusu umuhimu wa kuchangia damu, jambo lililowahamasisha wengi kushiriki.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Uhuru, Devotha Rweyemamu, ameushukuru uongozi wa JKT kwa hatua hiyo ya kuja kujitolea damu katika hospitali yetu kwani itaweza kusaidia wagonjwa mbalimbali waliopo hospitali hapo.

“Hospitali hii ipo barabarani, hivyo inapokea wagonjwa wengi wa ajali na huduma nyingine zinazohitaji damu kwa wingi. Hivyo msaada huu ni muhimu sana kwa wagonjwa wetu,” amesema  Devotha.

Aidha ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano wa JKT wa kufika katika hospitali hiyo kutoa msaada wa kutoa damu Salama.