Na OWM (KAM), Kigali
Waziri Mkuu wa Rwanda, Dkt. Justin Nsengiyumva, ameonyesha kuvutiwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Tanzania Bara na Zanzibar, baada ya kutembelea banda lao katika Maonyesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi - Jua Kali.
Ziara hiyo ilifanyika Novemba 3, 2026, ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa maonesho hayo katika Viwanja vya Gikondo, Kigali.
Dkt. Nsengiyumva alipata fursa ya kujionea bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na Watanzania na kuelezwa namna wajasiriamali hao wanavyotumia ubunifu na ujuzi wao kuzalisha bidhaa zinazoshindana ndani na nje ya nchi.
Akiwa bandani hapo, Waziri Mkuu huyo alikaribishwa na mjasiriamali Janeth Gabone, aliyemweleza kwa kina kuhusu aina ya bidhaa, ubunifu uliotumika na uwezo wa wazalishaji wa ndani kukidhi mahitaji ya soko.
Janeth alimwonyesha bidhaa mbalimbali zilizopangwa bandani hapo huku akifafanua namna zinavyotengenezwa na mchango wa wajasiriamali katika kukuza sekta ya uzalishaji nchini.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Nsengiyumva aliuliza maswali mbalimbali kuhusu bidhaa hizo na mahali zinapozalishwa. Janeth alimweleza kuwa bidhaa hizo zote zinazalishwa nchini, zikiwamo zinazotoka Zanzibar.
Waziri Mkuu huyo alionyesha kufurahishwa na kiwango cha ubora na ubunifu, na kuipongeza Tanzania kupitia wajasiriamali wake kwa ushiriki mzuri katika maonesho hayo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Godwin Mpelumbe, jumla ya wajasiriamali 350 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki maonesho ya mwaka huu, safari iliyoratibiwa na kuwezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita.




EmoticonEmoticon