THBUB NA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU KUIMARISHA USHIRIKIANO

November 25, 2026


Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe akiwa ameambatana na Makamu Mwenyekiti Mhe. Omar Ali Omar Bhai na viongozi waandamizi wa Tume hiyo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu na Watu, Mhe. Jaji Blaise Tchikaya katika makao makuu ya Mahakama hiyo Jijini Arusha leo Novemba 25, 2026. 

Ziara  hiyo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi katika kukuza na kulinda haki za binadamu nchini ni ya kwanza kufanyika mara baada ya uteuzi wa Viongozi hao wa  Tume uliofanyika Oktoba 28, 2026.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Wakili Mpelumbe amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu baina ya taasisi hizo katika kuimarisha ulinzi na heshima ya haki za binadamu.

Aidha, ameeleza nia ya THBUB kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Mahakama hiyo ili kuimarisha ushirikiano utakaowezesha kutekeleza shughuli za pamoja, kubadilishana uzoefu na maarifa, pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi hizo katika kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Tchikaya, amemshukuru Mwenyekiti wa THBUB kwa dhamira ya kuimarisha ushirikiano, akieleza kuwa mahusiano kati ya Mahakama hiyo na taasisi za kitaifa za haki za binadamu ni muhimu katika kukuza na kulinda haki za binadamu.

Aidha, Mhe. Jaji Tchikaya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano anaoutoa kwa mahakama hiyo kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake nchini na amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kutoa ushirikiano kwa Mahakama hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa zaidi za kubadilishana uzoefu na kuimarisha juhudi za pamoja katika kulinda haki za binadamu nchini.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »