TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA HAKI ZA BINADAMU,DEMOKRASIA NA UPATIKANAJI WA HAKI

November 06, 2026

GENEVA, USWISI | 5 NOVEMBA 2026

Tanzania imewasilisha hatua ilizopiga na maeneo ya kuendeleza katika kukuza na kulinda haki za binadamu, kuimarisha demokrasia, upatikanaji wa haki na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, katika Kikao cha Nne cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR) mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi.

Akiwasilisha taarifa ya nchi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mageuzi ya kisheria, kisera na kitaasisi kwa kuzingatia misingi ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4Rs), chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika eneo la upatikanaji wa haki, Waziri ameeleza kuwa Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria imewafikia takribani wananchi milioni 7.9, wakiwemo wanawake zaidi ya milioni nne. Aidha, sheria 446 zimetafsiriwa kwa Kiswahili ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kisheria na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao.

Katika kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, taarifa imeeleza kuwa uwakilishi wa wanawake Bungeni ulifikia asilimia 39.3 mwaka 2025, huku uwakilishi wao katika Mahakama ukifikia asilimia 36.5.

Katika sekta ya afya, taarifa imeonesha kupungua kwa vifo vya wajawazito kutoka 197 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000. Vilevile, asilimia 94.3 ya watu wanaoishi na VVU wamefikia kiwango cha kufubaza virusi, kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa.

Katika maendeleo ya miundombinu na huduma muhimu, umeme umefika katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara, huku kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kikifikia takribani asilimia 79.5.

Akizungumzia masuala ya demokrasia na matukio yaliyozunguka Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Mheshimiwa Ulega ametambua uzito wa matukio hayo na kueleza dhamira ya Serikali ya kubaini ukweli, kuhakikisha uwajibikaji na kulinda utu wa binadamu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Katika ushirikiano wa kimataifa, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuimarisha elimu ya haki za binadamu, kusambaza sheria kwa Kiswahili na kutumia teknolojia kwa uwajibikaji katika kuboresha huduma za umma.

Waziri Ulega amesisitiza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa kuendelea na mageuzi, kuimarisha taasisi na uwajibikaji, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na misingi ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma.

Ushiriki wa Tanzania katika mchakato wa UPR unaonesha umuhimu wa mazungumzo, uwajibikaji na ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu.

UNESCO National Commission of the United Republic of Tanzania (NATCOM Tanzania)

#Tanzania  #HumanRights  #UPR2026  #UNHRC  #NATCOMTanzania  #JusticeForAll

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »