LALJI FOUNDATION NA BARAKA FOUNDATION WAENDESHA KAMBI YA MATIBABU YA MACHO KWA ZAIDI YA WANANCHI 2,500 RUFIJI

November 16, 2026
LALJI FOUNDATION kwa kushirikiana na BARAKA FOUNDATION na VISION 4 ALL EYE CENTER imeendesha kambi maalumu ya matibabu ya macho bure katika maeneo ya Utete na Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, kwa siku tatu ambapo jumla ya wananchi 2,596 walifanyiwa uchunguzi na kupatiwa huduma mbalimbali za matibabu ya macho.

Kwa mujibu wa takwimu za kambi hiyo, wananchi 817 walipatiwa miwani, 1,360 walipatiwa dawa, huku wagonjwa 285 wakibainika kuhitaji huduma za upasuaji. Kati yao, wagonjwa 246 walikuwa na changamoto ya mtoto wa jicho (Cataract), huku 39 wakihitaji upasuaji mdogo.

Kati ya wagonjwa waliohitaji upasuaji, jumla ya wagonjwa 232 walifanikiwa kufanyiwa upasuaji, ambapo 209 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na 23 walifanyiwa upasuaji mdogo.

Akizungumza katika uzinduzi wa kambi hiyo, mganga mkuu wa mji wa Rufiji Dk. Mussa Rashid ambaye alimwakilisha mkurugenzi mtendaji alieleza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Aliipongeza LALJI FOUNDATION na BARAKA kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupeleka huduma za afya karibu na wananchi, akieleza kuwa mchango wa taasisi hiyo ni sehemu muhimu ya juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wale wenye uhitaji wa huduma za matibabu ya macho.

Aidha, aliomba kambi za matibabu ya macho ziwe zinafanyika mara kwa mara ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, akibainisha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma hizo katika jamii.

Pia, aliwahimiza wadau wengine wa maendeleo, taasisi binafsi na mashirika mbalimbali kujitokeza kushirikiana na Serikali katika kuwezesha kambi za matibabu na huduma nyingine za kijamii, akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya afya yanahitaji ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa LALJI FOUNDATION, Imtiaz Lalji, alieleza dhamira ya taasisi hiyo ya kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma za afya, hususan wale ambao wana changamoto ya kumudu gharama za matibabu.

Ameongeza kuwa kambi za matibabu ya macho ni sehemu ya mpango endelevu wa LALJI FOUNDATION katika kuchangia ustawi wa jamii, hivyo taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo ili kupunguza changamoto za magonjwa ya macho na kuwawezesha wananchi kupata huduma za matibabu kwa wakati.

Saida Minge Mkazi wa Ikwiriri aliishukuru LALJI FOUNDATION na wadau wote kwa kuwafikishia huduma karibu na maeneo yao, akieleza kuwa kambi hiyo imewasaidia kupata uchunguzi, dawa, miwani na upasuaji ambao kwa baadhi yao ungekuwa mgumu kuupata kutokana na gharama zake.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »