Na Mwandishi Wetu-Longido
Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu), Mamlaka ya Hewa Tanzania TMA pamoja na Shirika la Chakula Dunia (WFP) wametoa mafunzo kuhusu tahadhari ya kukabiliana na madhara ya El niño kwa Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha.
Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 08 Octoba, 2026 katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido ambapo mada mbalimbali kuhusu mfumo wa tahadhari, utabiri wa hali ya hewa ziliwasilishwa kwa Watendaji hao.
Kwa niaba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Longido, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Bw. Robert Urassa, wakati akifunga mafunzo hayo amewataka Watendaji hao kutoa elimu kwa wananchi juu ya uwepo wa mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni ili waweze kuchukua tahadhari za mapema na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
"Tunashukuru kuona Longido imechaguliwa kunufaika na mafunzo haya, kwa kuwa tunatarajia kupata mvua za juu ya wastani, tunaomba Kamati za Maafa za Kata na Vijiji na Maafisa Ugani mkawafikie wananchi kwa kuwapa elimu na kuwahamasisha kuchukua tahadhari mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza," amesisitiza Bw. Urassa.
Akiwasilisha mada kuhusu dhana ya usimamizi wa maafa na hatua za maandalizi ya kukabiliana na madhara ya El Niño Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Roman Mushi ametoa wito kwa watendaji hao kuhakikisha wanaporejea katika maeneo yao wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu uwepo wa mvua za El Niño na hatua stahiki za kuchukua kabla, wakatina baada ya mvua hizo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Nae, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Bi. Vaileth Masaba, akiwasilisha mada kuhusu huduma zinazotolewa na TMA, aina za utabiri wa hali ya hewa, maana ya El Niño, utabiri wa msimu, utabiri wa msimu kwa Halmashuri ya Wilaya ya Longido pamoja na namna ya kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii amesisitiza umuhimu na matumizi ya taarifa za tahadhari ya awali katika kujiandaa na kukabiliana na madhara ya mvua hizo.
Mbali na hayo Shirika la Chakula Duniani (WFP) imegawa vipaza sauti kwa watendaji wa Kata 15 za Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa lengo la kurahisisha utoaji wa elimu kwa wananchi na usambazaji wa taarifa za tahadhari ya awali kuhusu mvua hizo, aidha, Kata zilizonufaika na vipaza sauti hivyo ni Kata ya Ngereyani, Ketumbeine, Sinya, Namanga, Noondoto, Olmolog, Engarenaibor, Kimokouwa, Tingatinga, Ilorienito, Gelai Lumbwa, Gelai Meirugoi, Orbomba, Mundarara na Elang'atadapash.
Mafunzo hayo yamewakutanisha watendaji wa kata na vijiji, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ugani pamoja na viongozi wa dini na kimila kwa lengo la kuimarisha matumizi ya taarifa za tahadhari ya awali na kuongeza uwezo wa jamii katika maandalizi na mwitikio dhidi ya maafa yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño.











EmoticonEmoticon