Na. Mwandishi Wetu, Tabora
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa wito kwa watendaji wa uchaguzi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi, weledi na kujitoa ili kufanikisha zoezi la uchaguzi kwenye Jimbo la Chamwino na kata 11 za Tanzania Bara.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Dkt. Zakia Mohammed Abubakar Mkoani Tabora leo tarehe 01 Oktoba, 2026 wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 01 Oktoba, 2026.
“Ni matazamio ya Tume kwamba, baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino na Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara, unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Novemba, 2026,” amesema.
Dkt. Zakia amewakumbusha watendaji hao kuwa shughuli zote za uchaguzi zinaongozwa na Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi na maelekezo ya Tume na kuwasihi kuendelea kutenga sehemu ya muda wao kusoma Katiba, sheria na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ili yawaongoze katika kusimamia uchaguzi utakaokuwa huru na wa haki.
Amesisitiza kuwa ili ufanisi uwepo ni muhimu watendaji hao wakazingatia sifa na uwezo wakati wa kuteua na kuajiri watendaji wa vituo vya kupigia kura kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni.
“Kuhusu utaratibu wa kupata watendaji wa vituo, tunayo imani kuwa mtateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hii muhimu kwa mustakbali wa Taifa letu. Jambo hili limekuwa likisisitizwa tokea siku ya kwanza ya mafunzo kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni. Kazi ambayo inahitaji umahiri, umakini na weledi katika kuitekeleza,” amesema Dkt. Zakia.
Amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa mafunzo ya watendaji wa vituo yanafanyika kwa ufanisi na weledi katika tarehe zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.
Mafunzo hayo yamewahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.
Kata 11 za Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi wa Udiwani ni Nonde iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Nyingine ni Igalula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.
Mwisho.





EmoticonEmoticon