Serikali ya Uganda imepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, katika kuongoza juhudi za kuimarisha afyaya uzazi na ustawi wa wanawake, watoto na vijana barani Afrika na kupambana na magonjwa ikiwemo Malaria.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi wa Afya wa Uganda, Mhe. Anifa Bangirana, alipokutana na ujumbe wa Serikali ya Tanzania jijini Kampala, kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Waziri Bangirana amesema mapambano dhidi ya Malaria ni muhimu katika kuimarisha afya ya uzazi, kwa kuwa ugonjwa huo huathiri wanawake wajawazito na watoto hivyo kuongeza hatari ya vifo au athari zinazoweza kuzuilika.
Amesema kuwa Uganda inalenga kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030 kupitia Mkakati wa Kitaifa na Mpango wa Kutokomeza Malaria Busoga (Busoga Malaria Eradication Programme-BMEP), unaohusisha Serikali, wadau na jamii katika kutekeleza afua za kinga, upimaji na matibabu.
Taarifa ya utafiti wa viashiria vya Malaria nchini Uganda ya mwaka 2024/25 inaonesha kuwa matumizi ya kinga dhidi ya Malaria kwa wanawake wajawazito yameimarika, ambapo asilimia 73 walipata angalau dozi tatu za dawa za kinga, ikilinganishwa na asilimia 41 mwaka 2018/19. Hata hivyo, maambukizi ya Malaria kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59 imeongezeka kutoka 10% mwaka 2018/19 hadi 13% mwaka 2024/25, hali inayoonesha umuhimu wa kuimarisha juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania, Dkt. Sunday Dominico, Naibu Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika - Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ameeleza kuwa Rais Samia amekuja na lengo la Sifuri tatu kuelekea kuimarisha afya ya Mama na Mtoto ifikapo mwaka 2030.
“Rais Samia amelenga hadi ifikapo mwaka 2030 Bara la Afrika tuwe na Sifuri ya kujifungulia nyumbani, Sifuri ya vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, na Sifuri ya watoto wasiokuwa na chanjo” amefafanua Dkt. Sunday na kusisitizakuwa kuwa mapambano dhidi ya Malaria ni sehemu muhimu ya kufanikisha shabaha hizo na kulinda Afya ya Mama na Mtoto.
Akiongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika Mkoa wa Busoga, Dkt. Specioza Wandira Kazibwe, Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke wa Uganda (Mstaafu) na Mshauri Mwandamizi wa Rais wa Uganda kuhusu Idadi ya Watu na Afya amesema utafiti wa awali (pilot study) uliofanyika katika eneo la Busoga umeonesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya Malaria.
“Takwimu zinaonesha kupungua kwa msongamano wa mbu aina ya ‘Anopheles’ kwa asilimia 88.7, kiwango cha maambukizi mapya ya Malaria yaliyobainika katika vituo vya kutolea huduma za afya yameshuka kutoka 90% hadi 10%” amebainisha Dkt. Kazibwe na kuikaribisha Tanzania pamoja na wadau wengine kufika Busoga kujifunza namna walivyofanikisha programu hiyo.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania, ukiongozana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Meja Jenerali Marco Gaguti, umetembelea Kata mbalimbali katika Wilaya ya Iganga, Mkoa wa Busoga, kujifunza namna jamii inavyoshiriki katika utekelezaji wa Mpango wa BMEP katika kuimarisha afua za kinga na kudhibiti maambukizi ya Malaria.
EmoticonEmoticon