NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeipongeza Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi (TPFCS) kwa kupata cheti cha viwango vya kimataifa, hatua ambayo itasaidia kuimarisha mifumo ya taasisi na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhi cheti hicho, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa TBS, Dkt. Candida Shirima amesema kupata cheti hicho ni hatua muhimu katika kuboresha utendaji wa taasisi, lakini mafanikio yake yatategemea uwezo wa TPFCS kuendelea kuzingatia matakwa ya kiwango husika na kuhakikisha mifumo yake inafanya kazi kwa ufanisi.
“Kupata cheti ni hatua moja, lakini kukidumisha ni hatua nyingine. Lazima muendelee kutimiza matakwa yake, kufuatilia utendaji na kuhakikisha mifumo inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.
Dkt. Candida ameitaka TPFCS kuendelea kutafuta vyeti vingine vya kimataifa, huku akizihimiza taasisi za umma na binafsi kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa ili kuboresha huduma na kuimarisha weledi.
Amesema juhudi hizo zinaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha ufanisi, weledi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPFCS, Omari Issa, amesema bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa matakwa ya cheti kilichopatikana na kuhakikisha taasisi hiyo inapata vyeti vingine vya kimataifa.
“Nawahakikishia kwamba bodi itaendelea kusimamia kwa makini si cheti hiki pekee, bali pia vyeti vingine tunavyotarajia kupata katika kipindi kifupi kijacho,” amesema.
Aidha, ameiomba TBS kutumia fursa hiyo kuhamasisha taasisi nyingine ambazo bado hazijapata ithibati kuchukua hatua zinazostahili ili nazo zitimize matakwa ya viwango vya kimataifa.
Amesema kupata ithibati kwa taasisi nyingi kutasaidia kuimarisha ubora wa huduma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
EmoticonEmoticon