Na, Mwandishi wetu – Ankara, Uturuki
SERIKALI ya Tanzania imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Usimamizi wa Maafa na Dharura ya Uturuki (AFAD), kwa lengo la kuimarisha uwezo wa nchi katika kuzuia na kupunguza athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na dharura na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa kikao cha pamoja kati ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na uongozi wa AFAD kilichofanyika katika ofisi za taasisi hiyo mjini Ankara, Uturuki ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi nchini humo iliyolenga kuongeza ujuzi na maarifa ya kiufundi, kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kujifunza uzoefu wa Uturuki katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kujiandaa na kukabiliana na dharura, pamoja na kurejesha hali baada ya maafa kwa kutumia mbinu, mifumo na teknolojia za kisasa.
Dkt. Yonazi amesema Tanzania inathamini uzoefu na utaalamu wa AFAD katika usimamizi jumuishi wa maafa na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa manufaa ya Tanzania na Uturuki, hususan katika kuendeleza mifumo ya kisasa ya usimamizi wa maafa, teknolojia, mafunzo ya wataalam, utafutaji na uokoaji pamoja na uratibu wa hatua za mwitikio wakati wa dharura.
“Tanzania itaendelea kujifunza na kushirikiana na taasisi mbalimbali zenye uzoefu katika usimamizi wa maafa, ikiwemo AFAD, ili kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kuzuia na kupunguza athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali pindi yanapotokea,” amesema Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa AFAD nchini humo, Gavana Ali Hamza Pehlivan, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na Uturuki katika eneo la usimamizi wa maafa na kueleza kuwa AFAD ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya kitaalamu.
Gavana Pehlivan amesema maeneo hayo ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa maafa, mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya vihatarishi na madhara ya maafa, maandalizi na mwitikio wa dharura, pamoja na uanzishaji, mafunzo na uendelevu wa timu maalumu za utafutaji na uokoaji na upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika wakati wa maafa.
Ameeleza kuwa AFAD inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia dhana ya usimamizi jumuishi wa maafa, inayolenga kushughulikia hatua zote za mzingo wa usimamizi wa maafa, kuanzia katika kutambua na kutathmini vihatarishi, kuzuia na kupunguza uwezekano na athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na dharura hadi kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.
Vilevile, AFAD imejenga uwezo wa kuratibu timu za wataalam na vikosi vya utafutaji na uokoaji vinavyoshughulikia majanga mbalimbali, yakiwemo matetemeko ya ardhi, mafuriko na dharura nyingine, kwa lengo la kuokoa maisha na kulinda mali. Taasisi hiyo pia hushiriki katika uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa na kusaidia shughuli za kurejesha hali na makazi katika maeneo yaliyoathirika.
Katika eneo la kujenga uwezo wa rasilimali watu, AFAD inaendesha mafunzo na mazoezi ya vitendo kwa wataalam na timu za mwitikio wa maafa kupitia miundombinu yake ya mafunzo, ikiwemo Disaster and Emergency Training Centre (AFADEM). Mafunzo hayo yanalenga kuongeza ujuzi wa kitaalamu, uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja na utayari wa kukabiliana na matukio ya dharura.
Gavana Pehlivan ameongeza kuwa AFAD pia hushiriki katika ushirikiano wa kimataifa wa usimamizi wa maafa kupitia Timu ya Kimataifa cha Utafutaji na Uokoaji (The International Search and Rescue Advisory Group - INSARAG) ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UN-OCHA) katika kupeleka timu maalumu za utafutaji na uokoaji na kutoa msaada wa kibinadamu katika nchi mbalimbali pale kunapojitokeza maafa makubwa.
Tanzania na Uturuki zimeendelea kuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu katika eneo la usimamizi wa maafa, hususan katika teknolojia, mifumo ya taarifa na tahadhari za mapema, mafunzo, utafutaji na uokoaji, uratibu wa mwitikio wa kukabili na urejeshaji wa hali, kwa lengo la kujenga jamii na taasisi zenye uwezo mkubwa wa usimamizi wa maafa.

















EmoticonEmoticon