PROF.MKENDA ATOA WITO WA KUJENGWA MAKTABA ZA JAMII

October 20, 2026
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuandika na kuhifadhi historia, utamaduni na maarifa yake ili vizazi vijavyo viweze kujifunza kuhusu nchi yao kutoka katika vyanzo vilivyoandikwa na Watanzania wenyewe.
Prof. Mkenda amesema hayo Oktoba 20, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Nne la Kitaifa la Huduma za Maktaba na Tamasha la Vitabu na Usomaji, akisisitiza kuwa taifa lisipoandika hadithi yake lenyewe, kuna hatari ya historia na maarifa kuhusu Tanzania kutawaliwa na taarifa kutoka nje ya nchi.
Amesema Serikali itaendelea kusimama na waandishi wa Tanzania na kuunga mkono sekta ya uchapishaji katika kuhakikisha vitabu vinavyoandikwa  vinapata soko ikiwemo kuchapishwa na kusambazwa katika shule, maktaba na maeneo ya jamii.
Prof. Mkenda ameitaka Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania kuongeza ununuzi wa vitabu vya Watanzania na kuvisambaza katika maktaba mbalimbali, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ari na kuhamasisha uandishi nchini.
Aidha, amezitaka halmashauri na taasisi mbalimbali kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha maktaba za jamii, ili wananchi, hususan watoto na vijana, wapate maeneo ya kusoma na kupata maarifa. 
Amesema maeneo hayo yanaweza kuwa katika shule, taasisi za dini na maeneo mengine yanayofikika kwa urahisi jamii.
Akizungumzia Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Waandishi Bunifu, Prof. Mkenda amesema tuzo hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuchangamsha usomaji, kukuza uandishi na kuendeleza Kiswahili, huku akiwahimiza waandishi kutumia fursa hiyo kuwasilisha kazi zao na kushiriki katika kukuza sekta ya vitabu nchini.
Amesema Kongamano hilo linapaswa kuwa chachu ya kuendelea kukuza uandishi, usomaji na uhifadhi wa maandishi, akisisitiza kuwa Tanzania inapaswa kujiamini na kuhakikisha historia na hadithi zake zinaandikwa na kuhifadhiwa na Watanzania wenyewe kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ufunguzi wa Kongamano la Nne la Kitaifa la Huduma za Maktaba na Tamasha la Vitabu na Usomaji umeenda sambamba na uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Maktabawa Taifa kwa ajili ya kutambua na kuhifadhi machapisho yanayozalishwa nchini katika kumbukumbu za Taifa .
      

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »