Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa, amesisitiza umuhimu wa kuwafundisha watoto kutambua na kuelewa mazingira yanayowazunguka kabla na sambamba na kujifunza kusoma na kuandika, akisema hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuwajengea uwezo wa kuelewa maarifa wanayoyapata kupitia vitabu.
Akizungumza Oktoba 20, 2026, katika viwanja vya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, Posta, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mtahabwa alisema hayo alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Kitaifa la Huduma za Maktaba na Tamasha la Vitabu na Usomaji.
Alisema katika kukuza utamaduni wa kusoma, ni muhimu kuanza kwa kumsaidia mtoto kuelewa ulimwengu unaomzunguka, ikiwemo watu, vitu, shughuli na tamaduni, kabla na wakati anapojifunza kusoma na kuandika.
“Tunaposema vitabu na usomaji, ni vizuri tuanze na jambo moja muhimu sana katika maisha ya mwanadamu; kusoma ulimwengu kisha kusoma neno,” alisema Dkt. Mtahabwa.
Akifafanua zaidi, alirejelea dhana ya mwanafalsafa wa Brazil, Paulo Freire, kuhusu kusoma ulimwengu na kusoma neno, akisema mtoto anapopata uelewa wa mazingira yake, hujengewa msingi mzuri wa kuelewa na kutafsiri maarifa anayoyapata kupitia maandishi.
Alisema mazingira ya elimu ya awali yanapaswa kuandaliwa ili kuwawezesha watoto kujifunza kwa vitendo kupitia vitu halisi, watu na mazingira yanayowazunguka, sambamba na kuhamasishwa kusoma vitabu vya nakala ngumu na nakala laini.
“Tuwafundishe watoto kusoma vitabu sana, na tuanze kwa kuwafundisha kusoma ulimwengu,” alisema Dkt. Mtahabwa, akisisitiza kuwa kuwawezesha watoto kuelewa mazingira yao na kusoma vitabu kutawasaidia kupata maarifa, kukuza uwezo wa kufikiri na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ufanisi.
EmoticonEmoticon