MONDULI YAZINDUA MPANGO WA KUJIANDAA NA KUKABILIANA NA MAAFA

October 13, 2026


Na Mwandishi Wetu - Monduli

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Gloriana Kimath amezindua Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Halmashauri ya Wilayani ya Monduli ukiwa na lengo la kutoa miongozo na taratibu za kujiandaa na kukabili maafa katika halmashauri ya wilaya hiyo na hasa tunapoelekea katika mvua za msimu zinatotarajiwa.

Mhe. Kimath amezindua mpango huo sambamba na kufungua kikao kazi cha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Wilaya ya Monduli na kuimarisha utoaji wa matumizi ya taarifa za tahadhari za awali katika kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El Niño leo Oktoba 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo Mhe. Kimath amewataka Kamati za Usimamizi wa Maafa za Wilaya, wataalamu na wadau mbalimbali kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya kukabiliana na maafa.

“Katika juhudi za kuwa na utayari wa kukabiliana na majanga na usimamizi wa maafa kwa ufanisi, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli imeshirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kutambua umuhimu wa kuandaa Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa unaotoa mwongozo wa namna ya kuratibu na kusimamia upuguzaji wa vihatarishi vya maafa katika wilaya yetu” ameeleza Mhe. Kimath.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Salum Manyatta amesema kuwa, mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia matokeo ya Tathmini ya Vihatarishi na Uwezo wa wilaya wa kukabiliana na maafa, pamoja na historia ya matukio ya maafa yaliyoikumba Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.

“Mpango huu ni matokeo ya mchakato shirikishi uliohusisha taasisi na wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa katika ngazi ya wilaya hivyo tunatarajia mpango huu utawezesha masuala mbalimbali ikiwemo uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa katika hatua zote za usimamizi wa maafa (Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali)” amefafanua Dkt. Manyatta.

Aidha, Dkt. Manyatta amesisitiza kuwa, mpango huo utekelezwe usibaki kwenye makaratasi kwani ni nyenzo ya usimamizi wa maafa, hivyo unapaswa kuunganishwa na mipango, bajeti na shughuli za maendeleo za wilaya, pia Kamati za Usimamizi wa Maafa kwa kushirikiana na wadau  zihakikishe upatikanaji na utengaji wa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wake.

Nae, Mwakilishi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bi.Sandra  Hakim, amepongeza mamlaka za Halmashauri ya wilaya na wadau wote waliohusika katika kuandaa mpango huo.

“Hii ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha utayari na kuhakikisha kuwa tumejipanga vyema kulinda jamii na maisha ya watu pale majanga yanapotokea, tunapoelekea kwenye utekelezaji hitaji la kujumuisha  hatua za mapema katika mpango huu, maandalizi yasijikite katika kujua jinsi ya kukabili janga linapotokea bali pia kuhusu kuchukua hatua kabla halijatokea” amesema Bi. Sandra.

Tathmini ya vihatarishi iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli inaonesha kuwa halmashauri hiyo inakabiliwa na majanga makuu Matano ambayo ni ukame, mafuriko, migongano ya wanyamapori na binadamu, moto na ajali za barabarani.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »