BARRICK BULYANHULU YAFANIKISHA UJENZI WA SHULE MPYA YA MSINGI KIJIJINI BUSHINGWE

October 18, 2026

Sehemu ya jengo la Shule ya Msingi Bushingwe iliyojengwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa gharama ya Sh. milioni 388.3 kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bushingwe, iliyojengwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa gharama ya Sh milioni 388.3 kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), wakifuatilia masomo katika mazingira bora, salama na rafiki kwa ujifunzaji.

***
#Imeondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.


Katika Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga, utekelezaji wa miradi ya elimu kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu, kuimarisha usalama wa wanafunzi na kufungua fursa mpya, huku ukiwapa wananchi matumaini ya maisha bora.

Katika kutekeleza dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii zinazozunguka mgodi, Barrick Bulyanhulu imejenga Shule mpya ya Msingi Bushingwe, iliyopo katika Kijiji cha Bushingwe, Kata ya Bulyanhulu, kwa gharama ya Sh milioni 388.3 kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

 Shule hiyo inalenga kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta elimu na kuwawezesha kusoma katika mazingira bora na salama.

Ujenzi wa shule hiyo ulianza mwaka 2024 na kukamilika mwaka 2025. Shule ilianza kupokea wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza Januari 2026. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 395, ambapo 104 wanasoma elimu ya awali na 291 wanasoma darasa la kwanza.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Abdallah Daimu Hussein, amesema uwepo wa shule hiyo mpya ni faraja kwa wakazi wa Bushingwe na vijiji jirani, kwani umewarahisishia watoto kupata elimu karibu na makazi yao. 

Amesema shule hiyo imeongeza mwitikio wa wazazi kuwaandikisha watoto wao ikilinganishwa na hali ya awali, ambapo baadhi ya wanafunzi walilazimika kutembea umbali wa kilomita 10 hadi 15 kufuata huduma za elimu.

Baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo wameeleza kufurahishwa na mradi huo, huku wakitoa shukrani kwa mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa mchango wake katika kuboresha huduma za kijamii.

Ashura Khamis, mkazi wa Kijiji cha Bushingwe, amesema shule hiyo imewaondolea watoto adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu, hali iliyokuwa changamoto kubwa hasa kwa watoto wadogo.

“Kabla ya ujenzi wa shule hii, wanafunzi walilazimika kutembea umbali mrefu na ilikuwa kero kubwa, hasa kwa watoto wenye umri mdogo. Wazazi walilazimika kuwasindikiza shuleni na kwenda kuwafuata wanapotoka,” amesema Ashura.

Kwa upande wake, Juma Juma Marco amesema miradi ya CSR inayotekelezwa na Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Serikali imeleta manufaa kwa wanafunzi na wananchi kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na huduma nyingine za kijamii, ikiwemo afya.

Mbali na ujenzi wa shule hiyo, Barrick Bulyanhulu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ikijumuisha sekta za elimu, afya, ujenzi wa barabara na kilimo. 

Miradi hiyo pia inalenga kuwawezesha vijana, hususan wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mgodi, kupata fursa za kiuchumi na shughuli za kuwaingizia kipato.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »