WAKULIMA WA MKONGE WAKABIDHIWA VIWANDA

September 28, 2026

Na Oscar Assenga, Tanga

WAKULIMA wa zao la mkonge mkoani Tanga wamepata matumaini mapya ya kuongeza uzalishaji baada ya Serikali kuwakabidhi viwanda vidogo vya kuchakata zao hilo ili waweze kuzalisha na kuchakata wenyewe.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwa suluhisho la changamoto ya ukosefu wa mashine za kutosha za kuchakata mkonge, hali iliyokuwa ikisababisha zao hilo kuharibika baada ya kuvunwa kabla ya kufikishwa sokoni.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya awali ya makabidhiano ya viwanda hivyo kati ya Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Vyama vya Ushirika (AMCOS) vitano vya zao la mkonge Wilaya ya Korogwe, Shadrack Lugendo, alisema hatua hiyo itawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji.

Lugendo alisema makabidhiano hayo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Septemba 29, 2025, ya kuwakabidhi wakulima mashine ili waweze kuziendesha wenyewe.

Alisema Serikali imefanya uamuzi huo wakati muafaka kutokana na changamoto ambazo wakulima wamekuwa wakikabiliana nazo kwa muda mrefu.

“Tunaahidi uzalishaji utakuwa mkubwa zaidi na ile mikonge ya wakulima ambayo ilikuwa inakauka kwa sababu ya huduma za uchakataji tutaikamilisha, kwa sababu Bodi ya Mkonge inaendelea kuweka viwanda zaidi,” alisema.

Lugendo alisema hatua hiyo pia itawawezesha wakulima wadogo kushiriki moja kwa moja katika uchakataji wa zao hilo na kuongeza thamani yake.

“Matumaini yetu sasa ni kwamba uzalishaji utakuwa sehemu moja. Ili uzalishaji uwe mzuri zaidi, inatakiwa mwenye shamba ndiye aendeshe hizo korona. Sisi wakulima wadogo tunampongeza sana Rais kwa kuliona hilo ili kutoa nguvu zaidi kwenye uzalishaji wa zao la mkonge,” alisema.

Aliongeza kuwa tayari AMCOS mbili za Magoma na Magunga zimeanza kupatiwa mikopo itakayowasaidia kuboresha uzalishaji na kununua mashine za kuchakata mkonge.
BODI YATOA WITO

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saddy Kambona, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma katika zao hilo.

Kambona alivitaka AMCOS kuendelea kuwasimamia wakulima wadogo ili kuhakikisha wananufaika na kilimo cha mkonge na kuongeza uzalishaji.

Alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika zao hilo kutokana na mchango wake katika kuitangaza Tanzania kwenye soko la kimataifa, kuongeza Pato la Taifa na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

“Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma pale ambapo walikuwa wakifanya wenzetu wa SISALANA. AMCOS waongeze jitihada. Lengo la Serikali ni kuleta tabasamu kwa wakulima wadogo na Watanzania,” alisema.
NSSF YAWEKA WAZI

Naye Ibrahimu Maftaa, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF katika makubaliano hayo, alisema taratibu nyingine zinaendelea kukamilisha mkataba rasmi utakaowapa AMCOS chini ya usimamizi wa Bodi ya Mkonge mamlaka ya kuendesha mashine za kuchakata zao hilo.

Alisema awali shughuli hizo zilikuwa zikifanywa na SISALANA, kampuni tanzu ya NSSF.

“Tumeweza kusaini makubaliano ya awali kuweza kuendesha shughuli za mkonge ambazo zilikuwa zikiendeshwa na SISALANA na sasa tumewakabidhi TSB na AMCOS ambao wataweza kuendesha shughuli zote tulizokuwa tunazifanya,” alisema.

Alisema makubaliano hayo ni ya awali na kwamba taratibu zinaendelea kukamilisha mkataba rasmi utakaowapa AMCOS uwezo wa kuendesha shughuli zote za uchakataji wa mkonge.


Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »