TTCL YASISITIZA NAFASI YA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA 2050

September 29, 2026


Na MWANDISHI WETU - ARUSHA


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuimarisha nafasi yake katika kuwezesha shughuli za Serikali kidijitali kwa kutoa huduma ya intaneti yenye uhakika na kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano inayosaidia utekelezaji wa shughuli za Serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini.

TTCL imetoa huduma hiyo katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (Chairpersons and CEOs Forum), kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ambapo huduma ya intaneti imewawezesha washiriki kupata na kubadilishana taarifa kwa wakati, kufanya mawasiliano ya kidijitali na kutumia mifumo mbalimbali katika shughuli za kikao.

Kikao hicho cha siku tatu kimefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndenjembi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kinawakutanisha Wenyeviti wa Bodi, Wakuu wa Taasisi pamoja na viongozi mbalimbali kujadili masuala ya kimkakati yanayohusu uongozi, uwajibikaji, utawala bora na uboreshaji wa utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufunguliwa kwa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, amesema Shirika hilo litaendelea kuwezesha uchumi wa kidijitali kupitia uwekezaji na usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano, huduma za kifedha za kidijitali na teknolojia zinazochochea maendeleo ya taifa.

Bw. Marwa amesema miundombinu ya mawasiliano ina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kukuza uchumi wa kidijitali na kuwawezesha wananchi, wafanyabiashara na taasisi kupata huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Ameeleza kuwa TTCL inaendelea kuwekeza na kusimamia miundombinu ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, minara ya mawasiliano na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National ICT Data Centre), ambayo inawezesha upatikanaji wa mawasiliano, uhifadhi wa taarifa na matumizi ya huduma mbalimbali za kidijitali.

Kwa mujibu wa Bw. Marwa, jukumu la TTCL ni kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kujengwa, kuimarishwa na kusimamiwa kwa ufanisi ili huduma za mawasiliano zipatikane kwa uhakika na kusaidia shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema TTCL inachangia kuwezesha miamala ya kifedha ya kidijitali kupitia huduma zake, huku ikiendelea kuunga mkono juhudi za kukuza ajira kwa vijana kupitia programu za mafunzo kwa vitendo na kuwashirikisha katika shughuli za mawasiliano ya simu pamoja na usambazaji wa huduma za intaneti kwa teknolojia ya faiba kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akizungumzia matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), Bw. Marwa amesema teknolojia hiyo inahitaji miundombinu imara ya mawasiliano pamoja na uwezo wa kutosha wa kuhifadhi na kuchakata data.

Amesema TTCL inaendelea kuboresha na kupanua uwezo wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za kidijitali na teknolojia mpya.

Utoaji wa huduma ya intaneti katika kikao hicho unaakisi dhamira ya TTCL ya kuendelea kuwa mhimili wa mawasiliano nchini kwa kuiwezesha Serikali, taasisi na mashirika ya umma kupata miundombinu na huduma za mawasiliano zinazochochea ufanisi katika utendaji, ushirikiano na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kupitia uwekezaji katika miundombinu na uboreshaji wa huduma za mawasiliano, TTCL inaendelea kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Mageuzi ya Kidijitali Tanzania kwa kuhakikisha teknolojia inatumika kuongeza tija, uwajibikaji na ufanisi katika shughuli za Serikali na uchumi kwa ujumla.






Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »