Na Oscar Assenga,Tanga
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wana vifaa vya kutosha vya uokoaji ili kuwawezesha abiria kujinusuru wakati wa dharura.
Aidha, abiria wametakiwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na manahodha, hususan wakati chombo kinapokumbana na hitilafu au changamoto inayoweza kuhatarisha maisha yao.
Kauli hiyo hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kapteni Mussa Mandia, wakati wa mazoezi ya utafutaji na uokoaji wa abiria yaliyofanyika katika Bahari ya Hindi, mkoani Tanga.
Mandia alisema mazoezi hayo yalilenga kuonesha namna shughuli za utafutaji na uokoaji zinavyofanyika wakati wa dharura, huku akisisitiza umuhimu wa abiria kufuata maelekezo ya manahodha na kutumia vifaa vya kujiokoa.
“Hii ni sehemu ya kuonesha namna utafutaji na uokoaji wa abiria unavyofanyika wakati wa safari. Natumaini itawakumbusha madereva na abiria umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya nahodha, kuvaa vifaa vya kujiokoa na kutoa taarifa za dharura mapema,” alisema.
Aipongeza Serikali
Katika hatua nyingine, Mandia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua zinazochukuliwa kuboresha miundombinu ya usafiri na uchumi wa bahari nchini.
Alisema maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yameongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia meli kubwa, hatua aliyosema imeendelea kufungua fursa za kiuchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa.
“Tunaipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za kuboresha miundombinu ya usafiri na uchumi wa bahari. Maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga yameongeza uwezo wa bandari na kuleta matokeo chanya katika shughuli za bandari hii,” alisema.
Mandia pia alitaja hatua ya Serikali kuwezesha kupatikana kwa boti nne maalumu kwa ajili ya shughuli za utafutaji na uokoaji, ambazo zimewekwa katika maeneo mbalimbali likiwamo Bandari ya Tanga, Ziwa Victoria na Kigoma.
Alisema pia kuna boti maalumu ya kutoa huduma kwa wagonjwa iliyopo mkoani Mwanza.
Tanzania yazingatia mikataba ya IMO
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa maandalizi ya maadhimisho hayo yanayofanyika kitaifa mkoani Tanga, Stella Katondo, alisema Tanzania inaendelea kutekeleza mikataba ya kimataifa inayosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini (IMO) kuhusu utafutaji na uokoaji.
Katondo alisema Serikali imekuwa ikiandaa mazingira wezeshi yatakayosaidia kuimarisha usalama wa usafiri wa majini na kuhakikisha uokoaji wa maisha unakuwa kipaumbele wakati wa dharura.
“Tunafanya haya kwa kuzingatia kwamba Tanzania kama mwanachama tumeridhia mkataba wa kimataifa wa utafutaji na uokoaji unaosimamiwa chini ya SOLAS na IMO. Tuna wajibu wa kuokoa maisha kwanza, ndiyo maana tunazingatia taratibu zote,” alisema.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi inaendelea kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wenye weledi na wanaokidhi viwango vya kimataifa katika eneo la utafutaji na uokoaji.
Wataalamu kujiweka tayari
Naye Mkaguzi wa Meli za Kitaifa na Kimataifa pamoja na vyombo vidogo kutoka TASAC, Mhandisi Ally Diwani, alisema kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya usafiri wa majini, wataalamu wanapaswa kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kujiweka tayari kukabiliana na dharura.
Alisema mazoezi hayo ni muhimu katika kuhakikisha wataalamu wanakuwa tayari wakati wote kwa ajili ya kufanya shughuli za utafutaji na uokoaji pale inapohitajika.

EmoticonEmoticon