Na Mwandishi Wetu - Ankara Uturuki
SERIKALI ya Tanzania imesema inaendelea kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwamo satelaiti na akili unde (AI), ili kuimarisha tahadhari za mapema, mipango ya kujiandaa, kukabili na urejeshaji hali pindi maafa yanapotokea.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 28, 2026, na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa ziara yake ya kikazi mjini Ankara, Uturuki iliyolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kuongeza maarifa ya kiufundi na kukuza ushirikiano katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kukabiliana na dharura na mifumo ya kurejesha hali kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia.
Dkt. Yonazi ametembelea na kujionea namna Taasisi ya Turksat inavyotekeleza majukumu yake ikiwemo ya huduma za satelaiti, mawasiliano na teknolojia za anga ambayo inamilikiwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Uturuki. Turksat ndiyo mwendeshaji pekee wa satelaiti za mawasiliano nchini humo na hutoa huduma za data, interneti na mawasiliano kwa shughuli za kila siku za taasisi za umma na binafsi za ndani na nje ya nchi pamoja na maeneo ambayo miundombinu ya kawaida ni hafifu.
Katika kubadilishana uzoefu ameeleza kuwa, Tanzania inaendelea kuangalia namna ya kuongeza uwezo wa kutumia taarifa za satelaiti pamoja na teknolojia ya akili unde, hatua ambayo itasaidia kutoa taarifa za mapema kuhusu maeneo hatarishi na kuwezesha mamlaka kupanga namna bora ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kukabiliana na maafa.
Kwa mujibu wa Dkt. Yonazi, Ofisi ya Waziri Mkuu inalichukulia suala la kuzuia na kukabiliana na maafa kama jambo la kitaifa linalohitaji kujengewa uwezo wa kutosha katika maeneo yote ya nchi na si kuwa na uwezo wa kuokoa watu pekee wakati wa majanga, bali kuhakikisha usimamizi wa maafa unakuwa sehemu ya usalama wa nchi.
Akizungumzia matumizi ya teknolojia hiyo katika kukabiliana na mafuriko, Dkt. Yonazi alisema uwezo wa satelaiti unaweza kusaidia kutambua kina cha maji katika mito na maeneo yenye vihatarishi, pamoja na kutathmini ukubwa wa madhara yanayoweza kujitokeza.
Aidha, amesema kuwa taarifa hizo zitasaidia kuwezesha Serikali kupanga mapema rasilimali zitakazohitajika katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kuandaa rasilimali ikiwemo vifaa na timu kwenye maeneo yanayoweza kuathirika.
Akitoa maelezo kuhusu taasisi ya Turksat, Mkurugenzi wa huduma za satelaiti na mauzo Bw. Fuat Eroglu amesema taasisi hiyo ina sateliti sita angani na imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi yaliyogawanyika katika maeneo makuu matatu yanayohusu mawasiliano ya Satelaiti, huduma za mawimbi ya luninga na redio na data za interneti na Mifumo ya Teknolojia ya Habari kwa ajili ya Serikali Mtandao (e-Government).
Alisema pia taasisi hiyo inasambaza vifaa kwa ajili ya vituo vya huduma ya data za intaneti na mawimbi ya televisheni na redio kupitia satelaiti wakati wa maafa ili kuwezesha mawasiliano ya dharura pale ambapo minara ya simu na mkongo wa mawasiliano umeathirika.
“Kwa upande wa Mawasiliano ya Dharura na Kimkakati Turksat inatoa miundombinu salama ya mawasiliano kwa sekta za kimkakati kama vile usalama wa umma, jeshi, usafiri wa baharini, usafiri wa anga na mifumo ya mawasiliano wakati wa majanga ya asili au dharura,” alisema Eroglu








EmoticonEmoticon