SERIKALI YASISITIZA UMUHIMU WA KULINDA MAZINGIRA NA RASILIMALI ZA BAHARI.

September 22, 2026


 

Na Oscar Assenga, TANGA

SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na rasilimali za bahari, ikisema uharibifu wake unaweza kuhatarisha maisha ya wananchi, miundombinu na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotegemea bahari, mito na maziwa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar (SMZ), Mhandisi Ally Saidi Bakari, aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi wa Zanzibar wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Usafiri Majini Duniani  yaliyofanyika mkoani Tanga.

Mhandisi Ally amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za maji, ikiwemo bahari, mito na maziwa, ambazo zimekuwa nguzo muhimu ya ajira na kipato kwa wananchi kupitia uvuvi, utalii, biashara, usafirishaji, kilimo cha mwani na shughuli nyingine za uchumi wa bluu

Hata hivyo, amesema rasilimali hizo zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uharibifu wa mifumo ya ikolojia, mabadiliko ya tabianchi na matumizi yasiyozingatia uendelevu.

Amesema hali hiyo inahitaji ushirikiano wa Serikali, wananchi na wadau katika kuhakikisha mazingira ya bahari yanalindwa ili yaendelee kuwa chanzo cha fursa na maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Maji ni uhai, yawe baharini, mitoni au maziwa. Tusipoyaheshimu maji yatatushughulikia. Nguvu ya maji ni kubwa sana na tunapaswa kutambua umuhimu wake na kulinda rasilimali zilizopo,” amesema.

Ameonya kuwa uharibifu wa mazingira ya bahari unaweza kusababisha madhara makubwa, yakiwemo kupotea kwa rasilimali, kuathiri maisha ya wananchi na kuharibu miundombinu pamoja na makazi ya watu wanaoishi katika maeneo ya mwambao.

Kwa mujibu wa Mhandisi Ally, Tanzania inapaswa kutumia fursa zinazotokana na kuwa na bahari, mito na maziwa katika kukuza uchumi, huku ikiweka mkazo katika uhifadhi wa mazingira na usalama wa shughuli za usafirishaji majini.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari na usafirishaji wa majini, akiwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi za kuboresha miundombinu hiyo.

Ametaja maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Zanzibar na Bandari ya Tanga, pamoja na miundombinu ya usafirishaji katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, kuwa sehemu ya hatua zinazolenga kuongeza matumizi ya rasilimali za maji katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, amesema usalama wa vyombo vya usafiri majini unapaswa kupewa kipaumbele kutokana na kuwepo kwa ajali katika bahari, mito na maziwa.

Ametaka taasisi zinazohusika kuendelea kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini kabla na wakati vinapotumika ili kupunguza ajali na kulinda maisha ya abiria pamoja na mali zao.

Amesema maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yanatoa fursa kwa Serikali, wadau na wananchi kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya bahari na kutafuta suluhisho, ikiwemo namna ya kupunguza ajali za majini na kulinda mazingira.

TANGA

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, amesema kuchaguliwa kwa Tanga kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kunatokana na fursa nyingi za kiuchumi zinazopatikana kutokana na jiografia ya mkoa huo wenye mwambao wa bahari.

Mchatta amesema Tanga inaendelea kuwa kitovu cha shughuli za uchumi wa bluu, ikiwemo uvuvi, utalii, biashara na shughuli nyingine zinazohusiana na matumizi ya rasilimali za bahari.

Amesema maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Tanga yamechangia kuongeza shughuli za kiuchumi katika mkoa huo, akibainisha kuwa idadi ya meli zinazofika bandarini hapo imeongezeka hadi takribani meli 17 kwa mwezi, kutoka meli moja kwa mwezi katika kipindi cha nyuma.

Amesema ongezeko hilo limefungua fursa zaidi za biashara na shughuli nyingine zinazozunguka bandari, huku akitaja pia miradi ya kimkakati ikiwemo bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, kuwa miongoni mwa shughuli zinazoongeza umuhimu wa Mkoa wa Tanga katika uchumi wa nchi.

Hata hivyo, Mchatta amesema ongezeko la shughuli za bandari na uwekezaji linapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa mazingira ya bahari ili kuhakikisha fursa hizo zinaendelea kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.

Maadhimisho ya Siku ya Usafiri wa Majini Duniani yanatoa nafasi ya kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usafiri wa majini, usalama wa vyombo na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Kwa Tanzania, yenye bahari, mito na maziwa, rasilimali hizo zinaendelea kuwa muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii, jambo linaloifanya hifadhi na matumizi endelevu kuwa msingi wa kuhakikisha zinaendelea kuwa chanzo cha ajira, kipato na maendeleo.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »