DKT. YONAZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UTURUKI

September 30, 2026
Na, Mwandishi Wetu – Ankara Uturuki

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi ameupongeza Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki kwa kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kidiplomasia, biashara, uwekezaji, na maendeleo ya kijamii.

Dkt. Yonazi ametoa pongezi hizo alipotembelea Ofisi za Ubalozi huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mjini Ankara, Uturuki iliyolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kuongeza maarifa ya kiufundi na kukuza ushirikiano katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kukabiliana na dharura na mifumo ya kurejesha hali kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia.

Dkt. Yonazi amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki unazidi kuimarika kwa kasi kubwa, ukiongozwa na diplomasia ya kiuchumi, miongozo ya kimkakati kama vile Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ya Tanzania, pamoja na ziara za kitaifa za viongozi wakuu wa nchi hizo mbili.

Naye Kaimu Balozi Bi. Levina Maleo ambaye ni Mkuu wa Utawala wa ubalozi amempongeza na kumshukuru katibu Mkuu huyo kwa kutembelea ofisi za Ubalozi na kueleza kuwa wataendeleza mashirikiano yaliyopo kati ya nchi hizo mbili na kuendelea kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini hasa za elimu, afya na kijamii.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »