WAZIRI SANGU ASISITIZA NIDHAMU NA UADILIFU KWA BODI YA WADHAMINI PSSSF

August 01, 2026
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa HIfadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) jijini Dar es Salaam, Agosti 1, 2026.


Ataka Uwekezaji wenye Tija

Na: Mwandishi Wetu - Dar eś Salaam 

Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imeelekezwa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ili kuhakikisha mfuko unaendelea kuwa imara, endelevu na wenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wanachama.

Amesema hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mfuko huo wa PSSSF iliyofanyika leo Agosti 1, 2026, PSSSF Commercial Complex, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Sangu amesema jukumu kuu la bodi ni kusimamia shughuli za mfuko kama ilivyoainishwa katika Sheria ya PSSSF, kifungu cha 11 hususan katika maeneo makuu ya usimamizi ikiwemo huduma kwa wanachama, ukusanyaji wa michango, uwekezaji wa rasilimali za mfuko na ulipaji wa mafao.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Katikati) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa PSSSF jijini Dar es Salaam Agosti 1, 2026

Vile vile, amesisitiza kuwa katika kutekeleza majukumu hayo, bodi inapaswa kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na miongozo ya Serikali pamoja na Mpango Mkakati wa PSSSF, ambao umeanza kutekelezwa pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Wajumbe mmeingia katika kipindi muhimu ambapo mfuko umeanza kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano. Huu ndio utakaokuwa mwongozo wa utekelezaji wa majukumu na kufanikisha malengo ya mfuko,” amesema.



Kadhalika, amewataka wajumbe kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji, uwazi na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao, akibainisha kuwa Serikali ina matarajio makubwa kwa PSSSF katika kuhakikisha mfuko huo unakuwa imara.

Kuhusu uwekezaji, Waziri alisema fedha za wanachama zinapaswa kuwekezwa kwa umakini na weledi ili kulinda thamani yake na kuhakikisha zinazalisha faida itakayowezesha mfuko kutimiza wajibu wa kulipa mafao kwa wakati, hata baada ya miongo kadhaa.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo


“Fedha za wanachama zinawekwa leo kwa matarajio ya kulipa mafao miaka ijayo. Hivyo, ni muhimu ziwekezwe katika miradi yenye tija, salama na inayozingatia miongozo ya uwekezaji iliyowekwa na Serikali,” alisisitiza.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »