TRAMEPRO YAHIMIZA UNYONYESHAJI KWA AFYA YA MAMA NA MTOTO

Kajunason August 05, 2026
Dar es Salaam, Agosti 5, 2026 – Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa wito kwa Serikali, wataalamu wa afya, wataalamu wa tiba asili, wakunga, wadau wa mazingira na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kulinda afya na uhai wa mama na mtoto, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yanayoendelea kuanzia Agosti 1 hadi 7, 2026.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, TRAMEPRO limesema linaungana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika la Afya Duniani (WHO), UNICEF, Wizara ya Afya na wadau wengine wa afya duniani katika kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kama njia muhimu ya kuboresha afya ya watoto na akina mama.

Shirika hilo limeeleza kuwa Wiki ya Unyonyeshaji Duniani ilianzishwa mwaka 1992 na World Alliance for Breastfeeding Action (WABA) kwa ushirikiano na WHO na UNICEF, kufuatia Azimio la Innocenti la mwaka 1990, lenye lengo la kulinda, kuhamasisha na kuunga mkono unyonyeshaji wa maziwa ya mama duniani.

Kwa mujibu wa TRAMEPRO, unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni moja ya njia bora za kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuboresha afya ya mama. Shirika hilo limeunga mkono mapendekezo ya WHO yanayosisitiza mtoto kuanza kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, kupewa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza, na kuendelea kunyonyeshwa pamoja na vyakula vya nyongeza hadi miaka miwili au zaidi.

TRAMEPRO pia limebainisha kuwa Tanzania hupata wastani wa watoto kati ya milioni 2.2 na 2.4 wanaozaliwa hai kila mwaka, huku Afrika ikichangia takribani asilimia 70 ya vifo vya akina mama duniani. Aidha, zaidi ya watoto wachanga milioni moja hufariki kila mwaka barani humo kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, ikiwemo kuzaliwa kabla ya wakati, maambukizi, kukosa hewa wakati wa kuzaliwa na utapiamlo.

Shirika hilo limeeleza kuwa afya ya mama na mtoto haiwezi kutenganishwa na mazingira bora, likisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa maji safi, lishe bora, usafi wa mazingira, hewa safi na uhifadhi wa bioanuwai. Pia limefafanua kuwa mimea tiba, ambayo ni sehemu ya tiba asili, hutegemea mazingira salama na uhifadhi wa misitu pamoja na vyanzo vya maji.

Katika taarifa hiyo, TRAMEPRO limetoa wito maalumu kwa wataalamu wa tiba asili, wakunga wa jadi na wakunga wataalamu kuzingatia sheria, maadili ya taaluma na ushahidi wa kisayansi katika utoaji wa huduma. Pia limewahimiza kuwashauri wajawazito kuhudhuria kliniki mapema, kujifungulia katika vituo vya afya, kutambua dalili za hatari mapema na kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa afya ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Aidha, shirika hilo limetoa wito kwa Serikali kuendelea kuwekeza katika huduma za afya ya uzazi, kuongeza idadi ya wakunga na wahudumu wa afya, kuimarisha lishe, chanjo, maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na kuwekeza katika tafiti za tiba asili salama.

TRAMEPRO pia limealika Wizara, taasisi za Serikali, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kushirikiana katika kuendeleza tafiti, elimu ya afya, uhifadhi wa mimea tiba na ulinzi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Shirika hilo limemalizia kwa kusisitiza kuwa kulinda afya ya mama na mtoto ni jukumu la kila mwananchi na kwamba ushirikiano kati ya sekta ya afya, tiba asili na uhifadhi wa mazingira ni msingi wa kujenga Taifa lenye watoto wenye afya, akina mama salama na maendeleo endelevu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »