Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, amewasili jijini Dar kwa ziara rasmi ya siku mbili kuanzia tarehe 5-6 Agosti 2026, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Museveni pamoja na ujumbe wake amepokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye na viongozi waandamizi wa Serikali.

Akiwa nchini, Rais Museveni anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar Es Salaam, yatakayojikita katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, biashara, uwekezaji, miundombinu na sekta nyingine za kimkakati kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Ziara hii ni ya pili kwa Mheshimiwa Rais Museveni nchini Tanzania katika mwaka 2026. Ziara yake yakwanza ilifanyika Februari 2026, ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili, pamoja na utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) uliofanyika mwezi Machi 2026.

Ziara hii inatarajiwa kutoa msukumo mpya katika utekelezaji wa maamuzi yaliyokwishafikiwa na kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Uganda kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.


EmoticonEmoticon