Dodoma. Jumla ya taasisi za umma 54 zinatarajiwa kuwasilisha taarifa za utendaji wa uwekezaji mbele ya Kamati za Kudumu za Bunge kwa muda wa wiki tatu, katika mchakato unaolenga kuwezesha uchambuzi wa thamani na utendaji wa mitaji ya umma pamoja na utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya taasisi husika.
Katika awamu hii iliyoanza Jumatatu, Agosti 3, 2026, taasisi hizo zimepangwa kuwasilisha taarifa zao mbele ya Kamati mbili za Kudumu za Bunge, ambapo 27 zitawasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na nyingine 27 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC).
Hadi Jumatano, Agosti 5, 2026, taasisi nne zilikuwa tayari zimewasilisha taarifa zao mbele ya Kamati.
Taasisi hizo ni Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) na Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), huku Kamati zikionesha kuridhishwa na utendaji wa taasisi husika.
Uwasilishaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la kusimamia na kufuatilia utendaji wa uwekezaji wa Serikali kupitia taasisi na kampuni zilizo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).
OTR inasimamia taasisi na kampuni 308, zikiwemo taasisi za umma 252 na kampuni 56 ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, huku jumla ya uwekezaji katika taasisi na kampuni hizo ikiwa Sh92.3 trilioni.
Kaimu Msajili wa Hazina, Bi Lightness Mauki, alisema uwasilishaji huo unaipa Bunge fursa ya kupata picha ya kina kuhusu mwenendo wa uwekezaji wa mitaji ya umma.
“Uwasilishaji wa taarifa hizi ni moja ya utaratibu wa Bunge katika kusimamia Serikali, ikiwemo usimamizi wa uwekezaji wa mitaji ya umma,” alisema Bi. Mauki, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji wa Mashirika ya Kibiashara.
Taarifa hizo huwezesha kuangalia thamani ya mitaji, mapato na matumizi, faida, hali ya mizania pamoja na utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya taasisi husika, ikiwa ni msingi wa uwajibikaji na utawala bora,” alisema Mauki.
Uwasilishaji wa taarifa hizo unafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inayozipa Kamati jukumu la kuchambua na kubaini iwapo utekelezaji wa miradi ya uwekezaji wa umma unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu, sheria na miongozo ya biashara.
Kwa mujibu wa Bi. Mauki, Kamati pia inachambua na kujadili taarifa zinazohusu uwekezaji katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa.
Alisema OTR inaratibu mchakato huo na kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa zinaakisi kwa usahihi na uwazi hali halisi ya utendaji wa taasisi na mashirika ya umma, ili kuwezesha Kamati za Bunge kufanya uchambuzi na kutoa ushauri na maelekezo yanayolenga kuimarisha utendaji.
“Jukumu la Ofisi ya Msajili wa Hazina katika zoezi hili ni kuratibu na kuhakikisha taarifa za mashirika ya umma zinakuwa na ukweli na uwazi wa hali halisi wa utendaji wa taasisi hizo ili kutoa fursa kwa Kamati za Bunge kushauri na kuelekeza katika masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha utendaji wa mashirika ya umma,” alifafanua Mauki.
Uwasilishaji wa taarifa za mashirika hayo ulitanguliwa na uwasilishaji wa Taarifa kuhusu hali ya Uwekezaji wa Umma hadi kufikia Mwaka 2024/2025 mbele ya PIC.
Taarifa hiyo, iliyowasilishwa na Bi. Mauki, ilijikita katika kuonesha hali ya uwekezaji wa Serikali ndani na nje ya nchi, mgawanyo wa uwekezaji katika mashirika ya umma, mapato yasiyo ya kodi ya mashirika na taasisi za umma, mikopo ya mashirika na taasisi za umma pamoja na taarifa za dhamana na misaada katika mashirika hayo.
Mchakato huo unaendelea kutoa fursa kwa Bunge kuchambua mwenendo wa uwekezaji wa mitaji ya umma na kutoa maoni na maelekezo yanayoweza kusaidia kuimarisha utendaji, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya rasilimali za umma.



EmoticonEmoticon