Na Oscar Assenga, TANGA
VIJANA wameanza kutumia maarifa ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kubuni suluhisho za changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, kupitia mradi wa Vijana Bunifu unaotekelezwa chini ya programu ya Tanga Yetu
Mradi huo unaolenga kuwajengea watoto na vijana hamasa ya kujifunza masomo ya STEM, pia umekuwa ukitoa nafasi kwa vijana wenye mawazo ya kibunifu kuyabadilisha kuwa bidhaa au suluhisho zinazoweza kutumika katika maisha ya kila siku.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkufunzi wa Masomo ya STEM kutoka Project Inspire,Mohamed Mohamed, alisema lengo ni kuwajengea watoto na vijana msingi wa elimu ya STEM tangu wakiwa wadogo, huku wakiandaliwa kwa taaluma mbalimbali za baadaye.
Alisema Project Inspire inatekeleza mradi huo kupitia mfumo wa STEM Career Radar, unaolenga kumsaidia mtoto kutambua na kukuza uwezo wake katika nyanja za STEM, ikiwamo udaktari, uhandisi na Sayansi ya Kompyuta.
“Lengo letu ni kutengeneza interest kwa watoto katika kujifunza masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, kisha kuwasaidia kuchukua mawazo waliyonayo kichwani na kuyaweka katika uhalisia,” alisema Mohamed.
Alisema katika hatua ya kwanza, mradi unawahusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu hadi 12, ambao hufundishwa masomo ya STEM kwa njia ya vitendo ili kuwawezesha kuelewa kwa urahisi na kujenga hamasa ya kujifunza.
Kwa mujibu wa Mohamed, hatua nyingine inalenga vijana wenye umri wa miaka 13 hadi 18, ambapo vijana wenye mawazo ya kutatua changamoto mbalimbali katika jamii hupewa nafasi ya kuyafanyia kazi.
Alisema vijana hao hushiriki programu mbalimbali, ikiwamo Boot Camp, inayowapa fursa ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kutengeneza bunifu zinazolenga kutatua changamoto halisi.
Bunifu ya nyumba ‘inayohisi’ mvua
Miongoni mwa bunifu zilizotengenezwa na vijana hao ni mfumo wa nyumba unaoweza kutambua mvua na kusaidia kuzuia nguo zilizofuliwa na kuanikwa nje kutokulowana.
Mohamed alisema mfumo huo umewekewa kihisi (sensor) kinachoweza kutambua uwepo wa mvua.
Alisema mvua inapoanza kunyesha, mfumo huo hufanya kazi ya kupeleka sehemu ya kukaushia nguo upande ambao hauna mvua, hivyo kusaidia kuzuia nguo kulowana.
“Mfano, mtu amefua nguo na anatamani kuzivaa kwenye kikao, ametoka lakini mvua imeanza kunyesha. Mfumo unatambua kuwa kuna mvua na nguo zinarudishwa upande ambao hakuna mvua,” alisema.
Alisema mvua inapokatika, mfumo huo hutambua hali hiyo na kuirudisha sehemu ya kukaushia nguo upande wenye jua ili nguo ziendelee kukauka.
Mohamed alisema bunifu hiyo ni mfano wa namna vijana wanavyofundishwa kutumia STEM kutatua changamoto zinazojitokeza katika maisha ya kila siku.
Kutoka mshiriki hadi mlezi wa vijana
Kwa upande wake, Mboni Zahoro, mmoja wa wanufaika wa mradi huo, alisema safari yake ya kutumia STEM ilianza akiwa mwanafunzi na mshiriki wa programu ya Boot Camp.
Alisema baada ya kumaliza masomo, aliamua kujitolea na kujifunza zaidi namna ya kuwasaidia vijana wenzake kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukuza ujuzi wao.
Mboni alisema baada ya kuanza kwa mradi wa Vijana Bunifu alipata nafasi ya kuwa STEM Communicator, akitumia uzoefu na maarifa aliyoyapata kuwasaidia vijana wengine kukuza mawazo yao.
“Nilianza kama mwanafunzi na mshiriki wa Boot Camp. Baada ya kumaliza masomo nilijitolea kujifunza namna ya kuwasaidia vijana wenzangu kutekeleza sayansi, teknolojia na ubunifu,” alisema.
Alisema kwa sasa anawasaidia vijana kuchukua mawazo waliyonayo na kuyakuza kupitia teknolojia ili yaweze kuwa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mboni alisema anaamini kuendelea kuwafundisha vijana masuala ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati kutawasaidia kufikia mbali zaidi na kutumia ujuzi wao kuleta mabadiliko katika jamii.
Alisisitiza umuhimu wa vijana kujifunza kwa vitendo, akisema njia hiyo inawapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao, kukuza ubunifu na kutengeneza suluhisho zinazolenga changamoto halisi za jamii.
EmoticonEmoticon