📌_*Kamisheni ya Ardhi, ZRA na ZAECA yaweka kambi Nungwi kubaini ukiukwaji wa masharti ya umiliki wa ardhi katika mahoteli.*_
📌_*Ukaguzi waongeza ukusanyaji wa mapato na kuwezesha utoaji wa mikataba ya ardhi kwa wawekezaji.*_
Kamisheni ya Ardhi Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), imefanya ziara maalumu ya ukaguzi wa vibali vya ardhi kwa wawekezaji wa mahoteli katika Shehia ya Banda Kuu, Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kubaini ukiukwaji wa masharti ya umiliki wa ardhi na kuhakikisha ukusanyaji wa kodi ya ardhi unaimarishwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini A, Dkt. Farid Mohammed Haji @faridhaji_ , aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya Laila Burhan Ngozi, amesema ukaguzi huo umelenga kubaini wawekezaji wanaokiuka masharti ya umiliki wa ardhi, ikiwemo kutolipa kodi ya ardhi kwa Serikali.
Amesema ukaguzi huo umezaa matokeo chanya baada ya kuwabaini baadhi ya wawekezaji ambao hawakuwa wametekeleza wajibu wao wa kulipa kodi ya ardhi, hatua iliyowezesha mamlaka husika kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Mussa Kombo, amesema ukaguzi huo ni sehemu ya mkakati wa Kamisheni wa kuhakikisha wawekezaji wote wanatekeleza wajibu wao wa kulipa kodi ya ardhi kwa wakati na kuzingatia masharti ya umiliki wa ardhi. Ameeleza kuwa zoezi hilo pia limechangia kuongeza mapato ya Serikali kupitia malipo ya kodi ya ardhi, sambamba na utoaji wa mikataba ya ardhi kwa baadhi ya wawekezaji ambao hapo awali hawakuwa na mikataba hiyo.
Amesisitiza kuwa utoaji wa mikataba hiyo utaimarisha uwazi na uhalali wa umiliki wa ardhi, huku ukichangia usimamizi bora wa rasilimali za ardhi Zanzibar na kuhakikisha sheria za ardhi zinaendelea kuheshimiwa na kutekelezwa ipasavyo.



EmoticonEmoticon