
Katika juhudi za kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo 2034, Serikali katika mwaka wa fedha 2026/2027 itasambaza mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi 300 zinazolisha watu zaidi ya 100.
Hayo yamesemwa na Mtaalam kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, Bw. Omari Khalifa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (SabaSaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl.Nyerere jijini Dar es Salaam.
Khalifa amesema mpango huo utatekelezwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo jumla ya shilingi bilioni 15 ambazo ni fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.
Ameeleza kuwa mifumo itakayofungwa inajumuisha gesi ya LPG, majiko banifu, mkaa mbadala pamoja na majiko ya umeme kwa lengo la kuboresha huduma za upishi, kulinda mazingira na kuimarisha afya ya watumiaji.
Katika utekelezaji wa mpango huo kampuni mbalimbali zinazotoa huduma ya mifumo ya nishati safi ya kupikia zitafaidika kupitia fursa zitakazotangazwa na REA huku taasisi hiyo ikisimamia usimikaji wa mifumo hiyo katika taasisi zitakazokidhi vigezo vilivyowekwa.



EmoticonEmoticon