MTATIFIKOLO ASEMA SABASABA NI JUKWAA LA BIASHARA NA MAENDELEO

Kajunason July 02, 2026

 

Na Mwandishi Wetu

IRINGA – Mbunge wa Jimbo la Ismani, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo, amezindua rasmi maonesho na sherehe za Sabasaba zinazofanyika katika Kata ya Ilolo Mpya, Tarafa ya Pawaga, wilayani Ismani, huku akiwataka wananchi kutumia maonesho hayo kujifunza, kufanya biashara na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mtatifikolo alisema maonesho ya Sabasaba ni fursa muhimu kwa wananchi kukutana, kubadilishana uzoefu, kuuza na kununua bidhaa mbalimbali pamoja na kujifunza fursa za maendeleo kutoka kwa washiriki na wageni wanaotoka maeneo mbalimbali nchini.


Aliwahamasisha wananchi wa Kata ya Ilolo Mpya na Jimbo la Ismani kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo, akieleza kuwa mbali na burudani, maonesho hayo yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha mahusiano ya kijamii.

"Mnatakiwa kutumia maonesho haya kama jukwaa la kujifunza, kufanya biashara na kujenga mahusiano yatakayochochea maendeleo ya Ismani na wananchi wake," alisema Mtatifikolo.

Mbunge huyo pia aliwataka vijana kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani.



Aidha, aliwahimiza wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto katika misingi ya maadili, uzalendo na uwajibikaji ili kujenga kizazi kitakachochangia maendeleo ya taifa.

"Malezi bora ndiyo msingi wa kujenga taifa lenye vijana wenye nidhamu, uzalendo na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi," alisisitiza.

Maonesho hayo ya Sabasaba yanajumuisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, zikiwemo maonesho ya bidhaa, michezo ya mpira wa miguu, ngoma za asili pamoja na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.



Waandaaji wa maonesho hayo wamesema lengo ni kutoa fursa kwa wananchi kuonesha bidhaa na huduma zao, kuhamasisha biashara ndogondogo na kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo na sanaa.

Sherehe hizo hufanyika kila mwaka baada ya wananchi kumaliza shughuli za uvunaji, zikiwa sehemu ya kuimarisha mshikamano wa jamii, kuchochea biashara na kutoa burudani kwa wakazi wa Ismani na maeneo jirani.

Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walieleza kufurahishwa na maandalizi ya maonesho hayo, wakisema yameendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Jimbo la Ismani.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »