Moshi.
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imesema haijabadilisha matumizi ya eneo lolote la wazi, ikieleza kuwa kinachoendelea katika eneo la Uhuru Park ni utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kuboresha eneo hilo bila kuathiri matumizi yake ya awali.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alipozunguma kuhusiana na tetesi za kubadilishwa kwa matumizi ya eneo hilo.
Alisema kuwa, ofisi yake haijabadilisha matumizi ya ardhi katika eneo lolote na kudai baada ya Waziri Mkuu kuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufuatilia suala hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilitembelea eneo husika na taarifa ya uchunguzi itawasilishwa serikalini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Francis Shio, alisema eneo la Uhuru Park lina hati miliki ya halmashauri na tangu awali lilipangwa kutumika kama eneo la wananchi kupumzika na kufanyia shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema ujenzi unaoendelea wa vibanda vinavyozunguka eneo hilo ni sehemu ya mpango wa kulijengea uzio, kuweka mageti ya kuingilia na kutokea pamoja na kuimarisha usalama na mazingira ya bustani hiyo.
"Mpango huu si wa leo, miaka ya nyuma tayari halmashauri ilijenga vibanda takribani 39 katika eneo hilo. Sasa tunaendelea na hatua nyingine za utekelezaji wa mpango huo," alisema Shio.
Alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa uzio, eneo hilo litaboreshwa kwa ndani kwa kuweka sehemu za watoto kuchezea, maeneo ya mapumziko na huduma nyingine zitakazowezesha wananchi kulitumia kwa usalama zaidi.
"Lengo letu si kubadilisha matumizi ya eneo hili, bali kulifanya liwe salama na lenye huduma bora. Mzazi atakapomleta mtoto wake atakuwa na uhakika wa usalama kutokana na uwepo wa uzio," alifafanua.


EmoticonEmoticon