Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu akizungumza na Viongozi na Wananchi mara baada ya kukagua mradi wa Shule ya Msingi Mfinga iliyopo Sumbawanga, Mkoani Rukwa tarehe 19 Julai, 2026.
********************
Na: Mwandishi Wetu, Kwela
Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ametaka watumishi wa umma wote wanaodaiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Mfinga kufikishwa mahakamani haraka baada ya kubainika kuwepo kwa viashiria vya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akizungumza leo (Julai 19, 2026) baada ya kukagua mradi huo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kuhamasisha shughuli za maendeleo katika Jimbo la Kwela, na kueleza kuwa hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo licha ya fedha nyingi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake.
Ameeleza kuwa kati ya shilingi milioni 220.1 zilizotolewa kwa mradi huo tangu Julai 2025, tayari shilingi milioni 212.9 zimetumika lakini ujenzi bado haujakamilika jambo ambalo linaibua maswali kuhusu uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma.
“Fedha hizi zililetwa na Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto. Leo tunaelezwa na Mkaguzi wa Ndani kuwa mradi una hasara ya shilingi milioni 40. Siwezi kukubaliana na hali hii wakati waliohusika bado wako mitaani bila kuchukuliwa hatua,” alisema Sangu mbele ya wananchi.
Mbunge huyo amesema amepokea taarifa zinazoonyesha kuwa baadhi ya watu walikuwa wakipokea fedha kupitia akaunti zao binafsi na kuzitoa kwa matumizi yanayohusishwa na mradi huo kinyume cha taratibu za usimamizi wa fedha za serikali, akisisitiza kuwa tuhuma hizo zinapaswa kuchunguzwa kwa kina na wahusika kuwajibishwa.
Vilevile, amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wa kuwaandikia barua watumishi wanaotuhumiwa badala ya kuchukua hatua za kisheria. Alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Ephraim Konta kufuatilia kwa karibu jalada la uchunguzi lililopo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili hatua stahiki zichukuliwe.
Sangu amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini hivyo ni wajibu wa viongozi na watumishi kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa atazungumza na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Ally Chirukie ili kuhakikisha TAKUKURU inakamilisha uchunguzi wake kwa haraka na wale wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huo wanafikishwa mahakamani bila kujali nyadhifa zao.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mfinga Chrispin Costantino Ismail amesema fedha za mradi huo zililenga kujenga vyumba viwili vya madarasa ya elimu ya awali, vyumba sita vya madarasa ya shule ya msingi, matundu sita ya vyoo pamoja na uzio wa shule na kwamba mradi ulipaswa kukamilika Novemba 2025 lakini hadi sasa haujakamilika huku zikiwa zimebaki shilingi milioni 7.1 pekee.
Katika ziara hiyo Mhe. Sangu pia amekagua ujenzi wa shule shikizi ya msingi katika Kijiji cha Kipenzi Kata ya Mfinga ambapo aliahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji na mabati 100 ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo na kuwezesha shule kuanza kupokea wanafunzi mwaka ujao.
Ziara yake inaendelea katika Jimbo la Kwela ikiwa imelenga kukagua miradi ya maendeleo na kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kuendeleza shughuli za maendeleo jimboni humo.
Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu akikagua mradi wa Shule ya Msingi ya Mfinga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika jimbo hilo la Kwela, Sumbawanga, Mkoani Rukwa tarehe 19 Julai, 2026.




EmoticonEmoticon