Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa waandishi wa habari, wadau wa sekta ya habari na wananchi kupitia banda lake lililopo katika Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Huduma zinazotolewa ni pamoja na ugawaji wa vitambulisho vya ithibati kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, usajili wa waandishi wa habari, marekebisho ya taarifa za usajili pamoja na utoaji wa elimu kuhusu majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi hiyo.
JAB imesema ushiriki wake katika maonesho hayo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na wadau wa sekta ya habari, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma pamoja na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa ithibati na usajili wa waandishi wa habari nchini.
Bodi hiyo imewahimiza waandishi wa habari na wadau wengine kutumia fursa ya maonesho hayo kupata huduma kwa haraka na kwa ukaribu, huku ikieleza kuwa huduma hizo zinaendelea kutolewa pia katika Makao Makuu ya JAB.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanaendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazowasilisha huduma na bidhaa zao kwa wananchi.

















EmoticonEmoticon