WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), leo Julai 1, 2026, akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, pamoja na viongozi wengine, kwa lengo la kujadili uimarishaji na ukusanyaji wa mapato sambamba na uwekezaji katika Sekta ya Utalii na Maliasili.
Katika kikao hicho, Dkt. Kijaji alibainisha njia za kudhibiti na kuimarisha mapato katika Sekta ya Utalii, na kwamba utekelezaji wa mikakati hiyo itachangia kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa, kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za asili, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar amesema kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kubuni na kutekeleza mikakati madhubuti itakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali kupitia Sekta ya Utalii.
Aidha, kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA Mussa Nassoro Kuji; Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Yussuf Kabange, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Richie Wandwi, na viongozi wengine wa kisekta.





EmoticonEmoticon