NLD YAKEMEA WANAOWINDA URAIS 2030

June 03, 2026






Na Oscar Assenga, Tanga

CHAMA Cha National League for Democracy (NLD),kimeonya wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 kuelekeza nguvu zao katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi badala ya kuanza harakati za kisiasa mapema.

Onyo hilo limetolewa na  Katibu Mkuu wa Chama cha NLD Doyo Hassani Doyo wakati akizungumza na wabahabari Jijini Tanga baada ya kuhitimisha ziara ya kichama katika Mkoa wa Tanga, akieleza kuwa Taifa kwa sasa linahitaji mjadala unaolenga maendeleo na ustawi wa wananchi kuliko mjadala wa urais ambao muda wake bado haujafika.

Alisema ingawa Katiba na sheria za nchi zinatoa haki kwa kila mwananchi mwenye sifa kugombea nafasi yoyote ya uongozi, ikiwemo urais, si jambo la busara kwa viongozi kuanza kujinadi kisiasa wakati wananchi bado wanakabiliwa na changamoto nyingi za maendeleo.

Aidha alisema ni haki ya  kikatiba na kisheria kugombea nafasi yoyote ya uongozi lakini kwa mtazamo wake anaona jambo hilo sio lenye afya kwa Taifa kuanza mijadala ya urais miezi michache tu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika,.

Alidai kuwa katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge wa CCM wamekuwa wakitoa kauli katika Bunge na kwenye mikutano ya hadhara ambazo, kwa tafsiri yake, zinaashiria kuanza kwa harakati za kuwania urais wa mwaka 2030.

Kwa mujibu wa Doyo, viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wanapaswa kutumia nafasi zao kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuibua hoja zenye tija na kuishauri serikali katika masuala yatakayoboresha maisha ya Watanzania.

“Wananchi waliwachagua wabunge wao kwa matarajio ya kuona changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi. Tungetarajia kuona nguvu nyingi zikielekezwa katika kujadili maendeleo, uchumi, huduma za jamii na ustawi wa wananchi kuliko kujenga mazingira ya kampeni za uchaguzi ambao bado uko mbali,” alisema.

Aliongeza kuwa kuanza kwa siasa za urais mapema kunaweza kuathiri umakini wa viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao na hata kupunguza kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Doyo pia aligusia kauli mbalimbali zilizowahi kutolewa na baadhi ya viongozi wa serikali kuhusu watu wanaotamani nafasi ya urais mapema, akisema hali hiyo inaonyesha dalili za kuanza kujitokeza kwa makundi ya kisiasa ndani ya chama tawala kabla ya wakati wake.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa viongozi wa vyama vyote vya siasa wanapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kushirikiana kutafuta suluhisho la changamoto zinazowagusa wananchi katika maisha yao ya kila siku.

Katika hatua nyingine, Doyo aliwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kusimamia maendeleo ya nchi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Sasa ni wakati wa kushughulikia changamoto za wananchi, kuimarisha huduma za kijamii na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya taifa. Wakati wa siasa za urais ukifika, kila mwenye sifa na nia atapata nafasi ya kujitokeza,” alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa NLD Wilaya ya Tanga amesema bado kuna changamoto nyingi zinazohitaji ufumbuzi wa haraka mkoani humo, hususan katika sekta ya maji na miundombinu ya barabara.

Alisema viongozi wa chama hicho walijionea hali halisi ya baadhi ya maeneo wakati wa ziara yao, ambapo wananchi wengi bado wanakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama pamoja na miundombinu duni inayokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Alitaja baadhi ya barabara zinazounganisha maeneo ya Maramba, Mashewa, Korogwe, Mwakijembe na Lushoto kuwa miongoni mwa miundombinu inayohitaji maboresho ya haraka kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Tulipita katika maeneo mbalimbali na kujionea changamoto wanazokabiliana nazo wananchi. Bado kuna maeneo mengi yenye matatizo ya maji na miundombinu ambayo yanahitaji kipaumbele kutoka kwa mamlaka husika,” alisema.

Viongozi hao wa NLD walihitimisha kwa kuitaka serikali, viongozi wa kisiasa na wadau wa maendeleo kuelekeza nguvu katika kutatua kero za wananchi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wakisisitiza kuwa wananchi wanahitaji kuona matokeo ya maendeleo kuliko kushuhudia mijadala ya uchaguzi ambao bado uko miaka kadhaa mbele.

MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »