📌*Unalenga kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi*
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amezindua mfumo wa kidijitali wa kuagiza gesi ya kupikia uitwao Orion Gas, unaomilikiwa na kampuni ya Hygge, utakaowezesha wateja kuagiza mitungi ya gesi mtandaoni na kufikishiwa bila gharama za usafirishaji.
Mfumo huo utaanza kutumika katika mkoa wa Dar es Salaam kama sehemu ya kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi.
Akizungumza Juni 25, 2026 wakati akifunga Maonesho na Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia yaliyofanyika katika Ukumbi wa EACLC, Ubungo jijini Dar es Salaam, Mhe. Salome amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mkazo mkubwa katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo kuondoa baadhi ya kodi na ushuru kwenye vifaa vya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama kwa watumiaji.
Amesema juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau zimeanza kuzaa matunda ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.9 kwa sasa.
Mhe. Salome ametoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika uzalishaji na usambazaji wa teknolojia za nishati safi, taasisi za fedha kuweka mifumo rafiki ya mikopo kwa wafanyabiashara na wananchi, pamoja na vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa umma.
Ameeleza kuwa mwitikio mkubwa wa wadau wa ndani na nje ya nchi katika Maonesho na Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia unaonesha kuwa ajenda hiyo sasa imekuwa kipaumbele muhimu cha kitaifa. Amesema kongamano hilo limefanikiwa kuikutanisha Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika jukwaa moja la kujadili suluhisho za kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Katika hatua nyingine Mhe. Salome ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kushiriki Mbio za Kitaifa za Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking Marathon) zitakazofanyika Juni 27, 2026 jijini Dar es Salaam ili kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya, mazingira na ustawi wa jamii.





EmoticonEmoticon