Na WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Dkt. Gwajima amesema hayo Mei 22, 2026 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika Ukumbi wa Royal Village Hotel jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, Dkt. Gwajima amesisitiza kaulimbiu yake ya “Kasi Zaidi, Karibu Zaidi na Wananchi; Kasi Zaidi, Karibu Zaidi na Watumishi – KAZA KAZAWA,” akieleza kuwa inalenga kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi wa watumishi pamoja na kuimarisha mazingira bora ya kazi. Aidha, ameitaka Menejimenti ya Wizara kuendelea kutoa motisha kwa watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa ubunifu, weledi na kuzingatia maadili mema ya utumishi wa umma.
Aidha, Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha watumishi katika mijadala ya bajeti na utekelezaji wa mipango ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27. Vilevile, ametoa wito kwa watumishi kujiepusha na tabia hatarishi zinazosababisha maambukizi ya UKIMWI huku akiagiza Menejimenti kuendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi kazini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Chacha Maswi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha fikra chanya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia ngazi ya msingi ili kuhakikisha jamii inanufaika na huduma zinazotolewa kwa ufanisi. Amesema mafanikio ya Wizara yanategemea ushirikiano, uwajibikaji na ubunifu wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aidha, Maswi amesema Wizara itaendelea kuimarisha malezi ya familia pamoja na matunzo ya watoto ili kuhakikisha kizazi kinachokua kinapata maadili mema na mazingira bora ya maendeleo. Pia amesema Serikali imejipanga kuhakikisha makundi maalum yanapata huduma na fursa za kuwawezesha kukuza uchumi wao na kujitegemea kupitia programu mbalimbali za maendeleo ya jamii.
“Hatuwezi kuendesha taasisi kama mali binafsi, tunapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Maswi huku akiongeza kuwa Dira ya Taifa ya 2050 inahitaji watumishi wenye motisha, ubunifu na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kutoa matokeo chanya katika jamii.
MWISHO
.jpeg)
.jpeg)

EmoticonEmoticon