ARBAB VILLAGE IN TANGA KUFANYIWA MABORESHO MAKUBWA, CEO AMTAJA BAKHRESA

May 19, 2026

 



Na Oscar Asenga Tanga

Ikiwa ni zaidi ya miezi sita  tangu kuzinduliwa rasmi kwa Arbab Village mjini Tanga mnamo Desemba 6, 2025, eneo hilo sasa limeendelea kuwa gumzo kubwa kwa wakazi wa Tanga na wageni kutoka maeneo mbalimbali kutokana na muonekano wake wa kisasa, ubunifu wake wa kipekee na namna lilivyobadilisha kabisa taswira ya eneo hilo.

Mkurugenzi wa Arbab Village, Mbwana Imamu, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya muda mfupi ndiyo sababu kubwa iliyowasukuma kuanza mpango wa maboresho makubwa zaidi ili kufanya eneo hilo liendelee kuwa kivutio kikubwa zaidi ndani ya Tanga na nje ya Tanzania 🇹🇿 

Kwa sauti yenye kujiamini, Arbab amesema jambo lililompa nguvu zaidi ni namna wananchi wa Tanga walivyoikubali Arbab Village kwa haraka, tofauti na matarajio ya watu wengi waliokuwa hawaamini kama eneo hilo lingeweza kubadilika na kuwa sehemu ya kisasa yenye mvuto mkubwa wa biashara na burudani.

“Watu wengi hawakuwahi kufikiria kama hapa panaweza kuwa sehemu kama hii. Wapo waliowahi kujaribu kufanya uwekezaji lakini walishindwa. Mimi nilikuja na maono tofauti… niliamua kutumia ubunifu mkubwa na kufanya kitu ambacho watu watakikumbuka,” amesema Arbab.

Ameeleza kuwa hakutaka kufanya biashara ya kawaida kama zilivyo sehemu nyingine, bali alitaka kuleta utofauti ambao ungeifanya Arbab Village kuwa na hadhi yake ya kipekee ndani ya jiji la Tanga.

“Biashara kama hizi zipo sehemu nyingi, lakini nilikaa nikafikiria… nifanye nini ambacho kitawafanya watu wajisikie tofauti wakifika hapa? Ndiyo maana nikaja na ubunifu mkubwa ambao leo watu wameukubali na wengine kuvutiwa sana na kuiga”, amesema.

Kutokana na mwitikio mkubwa wa wateja kila siku, Arbab amesema tayari wameanza mipango ya kufanya maboresho makubwa zaidi yatakayoongeza hadhi na ubora wa huduma zinazotolewa katika eneo hilo.

Amesema maboresho hayo hayajasukumwa na malalamiko ya wateja, bali ni sehemu ya maono yangu  ya kuhakikisha kila anayefika Arbab Village anapata uzoefu bora na mpya zaidi.

“Sisi hatusubiri kuambiwa na wateja ndipo tubadilike. Tunataka kila siku tuwe bora zaidi kuliko jana,” amesema kwa msisitizo.

Katika mazungumzo yake, Arbab pia alitoa somo kwa vijana wanaotamani kuingia kwenye biashara, akisisitiza kuwa mafanikio hayapatikani kwa mihemko wala kushindana na watu, bali kwa kusikiliza mahitaji ya wateja na kuwa mbunifu.

“Ukitaka kuwa mfanyabiashara mzuri usipoteze muda kushindana na mfanyabiashara mwingine. Angalia wateja wako wanahitaji nini… hakikisha unawapa,” amesema.

Ameongeza kuwa vijana wengi wanaharibu safari zao za biashara kwa kuendeshwa na presha za mitandaoni na kutaka mafanikio ya haraka badala ya kujenga biashara kwa utulivu, ubunifu na uvumilivu, Arbab Village sio night club kwa maana tunapiga disco hapana, Arbab Village ni sehem tulivu yenye music wa wastan sio makelele huku ukipata chakula na vinywaji. 

Akizungumzia watu waliompa hamasa katika safari yake ya biashara, Arbab hakusita kumtaja mfanyabiashara maarufu wa Tanzania Said Salim Bakhresa kuwa mmoja wa watu waliomvutia kupitia maneno yake ya motisha.

“Niliwahi kumsikia Bakhresa akisema mfanyabiashara lazima ujaribu kila kitu na usikate tamaa. Pia lazima ujitume mwenyewe na upambane binafsi. Yale maneno yalinijenga sana,” amesema.

Arbab amesema leo hii wengi wanashangazwa na namna anavyofanikiwa kufanya mambo makubwa akiwa hana makundi ya vijana wenye mihemko au makelele, bali anaamini katika kazi, nidhamu, ubunifu na kujenga heshima ya biashara yake kupitia matokeo.

Kwa sasa, Arbab Village imeendelea kuwa moja ya sehemu zinazovuta watu wengi zaidi jijini Tanga, huku wengi wakisubiri kwa hamu kuona maboresho mapya yatakayofanyika katika eneo hilo ambalo tayari limeanza kubadilisha sura ya burudani na biashara ndani ya mkoa huo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »