Serikali imewataka Vijana wanaojishughulisha na Biashara za Mitandao nchini kuwa walinzi Wakuu wa mifumo ya kidijitali kwa kupambana vikali na matapeli wa mtandaoni, kwani vitendo vyao vinaharibu uaminifu ambao ndio nguzo kuu ya uchumi wa sasa na wa baadaye.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati akizungumza katika hafla kubwa ya 'Arise and Shine Recognition Rally 2026' iliyofanyika Mei 24, 2026 katika ukumbi wa The Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa kampuni ya BF Suma.
Katika hafla hiyo iliyokusanya zaidi ya vijana 30,000 waliojiunga na mfumo huo, Serikali imebainisha kuwa mustakabali wa ajira na masoko unahama rasmi kuelekea kwenye simu za mkononi, hivyo kulinda uaminifu wa wateja ni suala la kufa na kupona kiuchumi.
Londo amewaasa vijana kuvaa 'mabomu' (kujitoa kwa dhati) kupambana na wale wote wanaoharibu imani ya Watanzania kwenye biashara za kidigitali ili kulinda sekta inayotoa maelfu ya ajira.
Aidha, amewatoa hofu wadau hao kwa kueleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kufanya mabadiliko na maboresho ya Sera kwa lengo la kuijengea Sekta binafsi mifumo thabiti ya kibiashara itakayowapa vijana na wanawake fursa pana za kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali na biashara za mtandao (network marketing).
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Kiongozi wa Ngazi ya Juu wa 'The Gamechangers Team na BF Suma', Bw. Fadhili Mbogo, amesoma risala iliyobainisha vikwazo vikubwa wanavyokutana navyo ikiwamo baadhi ya watumishi wa Serikali wanaoshindwa kutofautisha makosa ya mtu binafsi na tasnia nzima ya biashara ya mtandao
Risala hiyo imefafanua kuwa jamii inakosa elimu ya kutofautisha kati ya kampuni halali ya biashara ya mtandao inayouza bidhaa halisi na kampuni za upatu ambazo kazi yake ni kutapeli wananchi na kuwarudisha nyuma kiuchumi.
















EmoticonEmoticon