NA EMMANUEL MBATILO,
WIZARA ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imeendelea kuimarisha udhibiti wa ubora wa bidhaa za chakula na vipodozi nchini kwa kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kupanua miundombinu ya maabara katika kanda mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo.
Waziri Kapinga amesema TBS imeanzisha ofisi katika kanda tisa nchini hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za viwango na kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa bidhaa sokoni.
Amesema pamoja na upanuzi huo, serikali imekamilisha ujenzi wa maabara katika Kanda ya Kati Dodoma na Kanda ya Ziwa Mwanza huku ikiendelea na taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya Kanda ya Kaskazini mjini Arusha.
“Wizara kupitia TBS imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi katika kanda tisa pamoja na ujenzi wa maabara katika maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema Kapinga.
Aidha, amesema wizara imeendelea kusajili bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi pamoja na zinazoingizwa kutoka nje ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Kapinga ameeleza kuwa TBS pia inaendelea kutoa ithibati kwa bidhaa za chakula na vipodozi kupitia tathmini na ukaguzi wa awali viwandani pamoja na kufanya ukaguzi endelevu wa bidhaa zinazouzwa sokoni.
Hatua hiyo, amesema, inalenga kulinda afya na usalama wa watumiaji sambamba na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.





EmoticonEmoticon