NA EMMANUEL MBATILO
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanikiwa kupata ithibati ya umahiri ya kiwango cha kimataifa cha ISO/IEC 17020 katika ukaguzi wa bidhaa, hatua inayotajwa kuwa chachu ya kuimarisha biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ameyaeleza hayo leo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (MB) wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, ithibati hiyo ilitolewa na Taasisi ya Huduma za Umahiri ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCAS), na kuifanya TBS kuwa taasisi ya kwanza nchini Tanzania na ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kupata hadhi hiyo ya kimataifa.
Amesema mafanikio hayo yanaashiria kuongezeka kwa uaminifu wa mifumo ya ukaguzi wa bidhaa nchini pamoja na kuimarisha uwezo wa Tanzania katika kudhibiti ubora wa bidhaa kwa viwango vinavyotambulika kimataifa.
“Ithibati ya umahiri wa mfumo wa ukaguzi katika kiwango cha kimataifa ni hatua muhimu na ya kimkakati inayoiwezesha nchi yetu kuepuka vikwazo vya kiufundi katika biashara, kuongeza kuaminika kwa matokeo ya udhibiti na kurahisisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi,” amesema Kapinga.



EmoticonEmoticon