📌 Vituo vitano vya CNG vinavyohamishika kununuliwa.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na sekta binafsi, inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa vituo 10 vya CNG (Gesi Asilia Iliyobanwa) nchini katika mikoa ya Dar es Salaam vituo nane, Mtwara kituo kimoja na Morogoro kituo kimoja.
Salome ameeleza hayo leo Mei 28, 2026, Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Arif Suleman Premji, Mbunge wa Mtwara Vijijini, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwekeza kwenye vituo vya CNG baada ya kuondoa ushuru wa shilingi 382 kwa kilo ya gesi ili kuhimiza matumizi ya CNG kwenye vyombo vya moto.
Salome amesema Serikali kupitia TPDC inakamilisha taratibu za ununuzi wa vituo vitano vya CNG vinavyohamishika (CNG Mobile Stations), kati ya hivyo vituo viwili vitawekwa Mkoa wa Dar es Salaam, kituo kimoja Mkoa wa Morogoro katika eneo la Chuo cha Ardhi, na vituo viwili Mkoa wa Dodoma katika maeneo ya Mji wa Serikali - Mtumba na Chako ni Chako.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea na ujenzi wa vituo vya CNG katika maeneo mbalimbali nchini, Kwa sasa kuna vituo 18 vya CNG vinavyofanya kazi katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Pwani.
Aidha, Salome amefafanua kuwa Serikali inaendelea na majadiliano na kampuni binafsi sita kwa ajili ya kuendeleza miradi midogo ya kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG) na kusafirishwa kwa magari maalum kwenda mikoa mbalimbali nchini ambayo haijafikiwa na miundombinu ya mabomba ya gesi asilia.
Amesema kwa mikoa iliyopitiwa na bomba la gesi, ikiwemo Mtwara, Serikali imejielekeza zaidi katika kusambaza gesi majumbani na kwenye taasisi kupitia mabomba ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wananufaika na rasilimali hiyo.




EmoticonEmoticon