NLD YATETEA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI

May 24, 2026

 



>Sheria Isichague Chama

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema mjadala unaoendelea kuhusu hatua zinazochukuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa umeonyesha jinsi baadhi ya Watanzania wanavyotoa hukumu za haraka bila kutafakari misingi ya sheria.

Doyo alisema kumekuwa na mtazamo kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inalenga zaidi vyama vya upinzani, huku ukweli ukiwa ni kwamba taasisi hiyo inasimamia sheria bila kuangalia itikadi ya chama husika.

Akizungumza wakati wa ziara ya chama hicho mkoani Tanga, alisema hatua zilizochukuliwa hivi karibuni dhidi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa zinatokana na matamshi yaliyotafsiriwa kuwa na viashiria vya uvunjifu wa sheria za vyama vya siasa.

“Sheria iko wazi. Chama au kiongozi anayekiuka taratibu anaweza kupewa adhabu ya faini, kusimamishwa shughuli au hata kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria. Hii siyo kwa chama fulani pekee,” alisema.



Alieleza kuwa baada ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoa kauli zilizozua mjadala, Ofisi ya Msajili iliwaandikia barua ya kutaka maelezo. Hatua hiyo, kwa mujibu wa Doyo, ilitafsiriwa vibaya na baadhi ya wananchi pamoja na wanaharakati waliodai kuwa upinzani unaonewa.

Hata hivyo alisema hali hiyo imebadilika baada ya mmoja wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) naye kuandikiwa barua kufuatia matamshi yake ya kisiasa.

“Watu walidhani sheria inafanya kazi kwa upande mmoja, lakini sasa imeonekana wazi kuwa anayevunja sheria ndiye anayechukuliwa hatua, bila kujali anatoka chama gani,” alisema.

Doyo alisema vyama vya siasa vinapaswa kutambua kuwa vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na hivyo vina wajibu wa kuendesha shughuli zake ndani ya mipaka ya kisheria.

Alionya kuwa siasa zisizo na nidhamu zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa Taifa.

“Ukianza kufanya siasa nje ya sheria, maana yake unaondoka kwenye misingi ya kisiasa na kinachofuata ni migogoro na vurugu. Taifa haliwezi kujengwa kwa misingi ya shinikizo na vitisho,” alisema.



Aidha, aliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kusimamia sheria kwa uthabiti bila kuogopa presha za kisiasa kutoka kwa wanasiasa au wanaharakati.

Kwa mujibu wa Doyo, uwepo wa taasisi imara zinazotekeleza sheria kwa haki ndiyo msingi wa kulinda amani na utulivu wa nchi.

Katika ziara hiyo ya NLD iliyoanzia Pangani na kuelekea Lushoto, chama hicho kimesema kinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za kisiasa ili kuimarisha demokrasia na mshikamano wa Taifa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »